Habari za Punde

MTAALAMU AWATAKA WAATHIRIKA WA MATENDE WAFUATE MAELEKEZO

Na Rahma Suleiman

WANANCHI walioathirika na maradhi ya matende wametakiwa kuhakikisha kuwa wanafuata maelekezo waliyopewa na wataalamu wa maradhi hayo ili kujinusuru na maambukizo ya maradhi mengine.

Hayo yalielezwa na mzamini wa kituo cha afya cha maradhi ambayo hayakupewa kipaumbele Dk. Khalfani Abdallah Mohammed alipokua akizungumza na muandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Lumumba wilaya ya mjini Unguja.

Alisema kuwa maelekezo ya wataalamu kunapelekea kudhibiti maradhi hayo ambayo yalishamiri zaidi katika maeneo ya wilaya ya Kusini Unguja na eneo lililoongoza ni Kizimkazi.

Dk. Khalfani alisema kuwa kitengo hicho kimefanya jitihada ya kutoa elimu kwa kuwashirikisha wanasiasa, viongozi wa dini, masheha na wananchi wenyewe ili kuweza kuwashajihisha na kuhakisha maradhi hayo yanaondoka.

Aidha alifahamisha kuwa waliweka msimamo maalum wa kuwasajili watu wenye maradhi hayo kila wilaya kwa kufanya warsha mbalimbali za kuelimisha jinsi ya kujikinga na maradhi hayo.

Hata hivyo alisema kuwa waliweka mpango maalum wa kutoa dawa kwa wananchi kwa kila baada ya miaka sita tangu walipoanza kutafuta ufumbuzi wa maradhi hayo kwa kutoa tiba.

Sambamba na hayo Dk. huyo aliwataka wananchi kuachana na dhana potofu ya kwamba dawa hizo zinaharibu uzazi bali wafahamu kuwa dawa hizo ni kwaajili ya kinga ya maradhi hayo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.