Na Ramadhan Himid, POLISI
WANANCHI wa Chuini wilaya ya Magharibi Unguja wamelalamikia uongozi wa baa ya Fuji kushindwa kuwadhibiti watoto wadogo ambao hufika huko kupata vinywaji jambo ambalo linapelekea watoto wengi kupotea kimaadili.
Malalamiko hayo waliyatoa mbele ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama kilichofanyika kijijini humo.
Akitoa malalamiko hayo Asha Salum Mohammed alisema watoto wadogo wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya ulevi na kudiriki hata kuwaibia wazazi wao ili wapate pesa za kwenda kulewa baa ya Fuji.
“Sisi wananchi wa Chuini tuna malalamiko kwa baa ya Fuji na sio kwamba tuna chuki nayo lakini tunachotilia mkazo ni kwamba wawadhibiti watoto wadogo wasiingie kwenye baa hiyo ili kuwanusuru watoto hao kuingia katika vitendo vya kihalifu kwani hivi sasa wamefikia hatua hata kutuibia pesa ili wapate kwenda Fuji”, alisema.
Aidha wananchi hao wamelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi yakinifu kuona kama baa hiyo ina kibali cha kuuza ulevi pamoja na kutowaruhusu watoto wadogo kuingia kwenye baa hiyo ili kunusuru vijana kutumbukia katika vitendo vya kihalifu.
Hata hivyo wamevitaka vyombo vyengine vya sheria vinavyohusika na utoaji wa vibali vya vileo kuandaa mikakati maalum na kupiga marufuku watoto wadogo kuingia kwenye baa vyenginevyo watoto wanaweza kuharibika mno kimaadili.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema malalamiko yao ni ya msingi na atahakikisha kuwa watoto hao wanadhibitiwa kuingia kwenye baa pamoja na kumbi za starehe lakini hayo yote yatafanikiwa iwapo kamati yao ya ulinzi, usalama na ustawi wa jamii itafanya kazi kikamilifu.
Alisema iwapo Kamati hiyo itafanya vikao, kutoa taarifa mbali mbali na kuzijadili kwa kuzipatia ufumbuzi watafanikiwa kuondosha kero mbali mbali kwani kuna mifano mingi ya Shehia zilizofanikiwa kupunguza uhalifu kupitia Kamati hizo.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi, usalama na ustawi wa jamii Shehia ya Kwaalinato, Mussa Idrissa Majura alitoa mfano wa Baa ya ‘Intro’ ambayo ilikuwa ikilalamikiwa kwa kila aina ya vitendo viovu lakini vitendo hivyo vimepungua kutokana na kamati yao kufanya kazi ipasavyo.
“Nikwambieni wananchi wa Chuini, sisi Kwaalinato hatujafanikiwa kupunguza uhalifu si kwa uhodari wetu bali mashirikiano ya wanashehia wenyewe ndio yaliyotufanya leo hii tupo hapa tunajigamba”.
Alisema vurugu zilizokuwa zikisababishwa na baa hiyo vilisababisha mtoto mdogo kuuawa lakini baa hiyo hivi sasa imeondoka.
No comments:
Post a Comment