SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO), limetangaza mgao mpya wa uzimaji wa umeme utaanza saa 12 jioni hadi saa tano za usiku kuanzia Mei 19 hadi 23 mwaka huu kwa Unguja nzima.
Akitangaza mgao huo mbele ya waandishi wa habari, Meneja Uendeshaji wa ZECO, Abdallah Haji Steni huko katika ukumbi wa Shirika hilo, Gulioni mjini hapa.
Alisema mgao huo utakuwa unaendeshwa kuanzia 12:00 za jioni hadi saa 1:15 kwa zone mbili za mwanzo na baadae kuendelea na zone nyengine hadi saa 5:00 usiku ambapo utakuwa kwa muda wa saa moja na robo kwa kila zone, ambapo kisiwa cha Pemba hawatohusika na zoezi hilo kwa vile kuna matumizi madogo ya umeme.
Alisema mgao huo unatokana Shirika la TANESCO kufanya matengenezo makubwa katika mtambo wa gesi Songosongo wa jijini Dar es Salaam na kusababisha kupungua kwa nguvu za umeme nchini, ambapo mgao wa Zanzibar utakuwa megawati 30 kwa kipindi hicho hadi wamalize matengenezo hayo.
Alieleza Zanzibar ilikuwa inapokea umeme megawati 45 kulingana na uwezo wa waya wake lakini hivi sasa matumizi yameongezeka hadi kufikia megawati 50.
Meneja huyo, alifahamisha kutokana na upungufu huo ZECO litafanya mgao wa umeme nyakati za usiku kwa vile ndio kwenye matumizi makubwa ya huduma hiyo kuanzia Mei 19 hadi 23 na baadae watatoa taarifa nyengine.
Mapema Ofisa wa Uhusiano wa ZECO, Salum Abdallah Hassan alifafanua kuwa, mgao huo upya utaukumba zone ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na Fumba ambazo katika mgao wa mwanzo zilikuwa hazimo kutokana na kuwepo kwa matumizi madogo lakini hivi sasa zinaingizwa kutokana na upungufu mkubwa wa megawati zinazotoka katika Gridi ya Taifa Tanzania Bara kuja Znzibar.
Alizitaja zone hizo ni pamoja na Kaskazini inakuwa peke yake kwa vile kuna matumizi makubwa ya umeme, ambapo mgao huo utaukumba hadi kisiwa cha Tumbatu.
Aidha zone ya Kusini itakuwa na zone Saateni 5, Zone ya Fumba itakuwa na COTEX, Mtoni Mpendae na Saateni 6, ambapo umeme utazimwa kila siku.
Alisema mgao uliokuwa ukifanyika awali baadhi ya siku katika wiki umeme ulikuwa hauzimwi siku tatu kulingana na zone zilivyopangwa kutokana kupungua kwa matumizi ambapo Mei 19 utazimwa mfululizo.
No comments:
Post a Comment