Mwantanga Ame
KAMATI ya Baraza la Wawakilishi ya Mifugo, Uwezeshaji, Utalii na Habari imeitaka wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, kuzisimamia Idara zake zote pale zinapofunga mikataba.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Asha Bakari Makame alieleza hayo hoteli ya Swahili Beach, kwenye majumuisho ya kamati hiyo ambayo ilifanya ziara ya kuzitembelea Idara mbali mbali za Wizara hiyo.
Kamati hiyo imeitaka wizara hiyo kuhakikisha inasimamia mikataba inayofungwa na Idara zake na suala hilo lisiachwe kwa Idara hizo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa baadhi ya Idara Wizarani humo kufunga mikataba bila ya wizara kujua na kuwepo kwa kasoro za kisheria kwenye ufungwaji wa mikataba hiyo.
Alisema wizara lazima iingilie suala la ufungwaji wa mikataba kwenye Idara zake kutokana na baadhi ya watendaji wa Idara hizo kutumia mwanya wa kutumia vibaya fedha za serikali kwa kazi za ujenzi, huku pia zabuni hizo zikiangukia kwenye kampuni zisizo na sifa.
Akipiga mfano Mwenyekiti huyo alisema Mkandarasi aliepewa kujenga Chuo cha Utalii kilichopo Maruhubi ambapo hafahamiki na haieleweki ni nani alihusika kutiliana saini mkataba wa ujenzi kwa wale waliomrithi nafasi za sasa.
“Jamani angalieni hii ni hatari kubwa kwani hata hawa waliochaguliwa sasa wanafika hapo hawajui hata huo mkataba ni nani aliyetiliana saini na mjenzi, huu ni ubabaishaji mkubwa wa kutumia vibaya fedha za serikali” alisema Mwenyekiti huyo.
Eneo jengine lililobainika kuwa na hitilafu katika wizara hiyo ni utata wa mikataba hoteli ya Bwawani baada ya baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kamati hiyo kuhoji uhalali uliotumika katika ukodishwaji wa ukumbi wa disko kwa bei ya chini na kuacha bei ya juu.
Aidha Mwenyekiti huyo aliutaka uongozi wa wizara hiyo kuona suala la kuyashughulikia majengo ya kumbukumbu ili yabakie katika uhalisia wake ikiwa pamoja na mapango kutokana na sekta ya utalii kuyategemea sana maeneo hayo katika kukuza utalii hapa nchini.
No comments:
Post a Comment