Habari za Punde

MTENDE KUMZUIA ANAEPORA ARDHI

Na Ameir Khalid

WANANCHI wa kijiji cha Mtende Wilaya ya Kusini Unguja wamepanga kumzuia kuingia katika kijiji hicho mwananchi anayedaiwa kuhodhi ardhi ya kijiji hicho kinyume na sheria.

Wananchi hao walisema watatekeleza dhamira ya kumzuia kuingia kijijini hapo mwananchi huyo, kwa kile walichodai kudharauliwa na vyombo husika juu ya madai yaliyowasilishwa katika taasisi kadhaa wakilalamikia kuporwa ardhi yao.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao walisema muda mrefu umepita, tangu pale walipopeleka malalamiko yao kwa vyombo husika ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kusini, lakini hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa.

“Tumepeleka malalamiko yetu tangu mwaka jana, hakuna jijitihada zozote ambazo tumeona zimechukuliwa, kwa hivyo sisi tumeamua kwa umoja wetu kumzuwia mtu huyo asiingie kijijini mwetu kwani wao wameshindwa kumzuwia’’,walisema.

Walifafanua kuwa mtu huyo ambaye ameshirikiana na mmoja ya wazaliwa wa kijiji hicho wameamua kuchukuwa eneo kubwa la ardhi karibu na ufukwe, bila ya kufuata sheria za kijiji jambo ambalo limeleta suitafahamu baina ya wanakijiji hao na mtu huyo.

Walisema kuwa siku za awali walipoona mtu huyo tayari ameshachukuwa eneo hilo walifika Ofisini kwa Mkuu wa wilaya ya Kusini kupeleka malalamiko yao, na kuahidiwa kuwa suala hilo linafanyiwa kazi, na wao ndipo walipoingia moyo na kuamua kusubiri maamuzi ya viongozi wao.

“Walitutia moyo pale walipotwambia suala hilo linafanyiwa kazi na sisi tukaamua kuwa watulivu tukisubiri maamuzi yao, lakini ni muda mrefu umekwenda hakuna chochote kile ambacho kinaendelea, tena baya zaidi ni pale mtu huyo anapoendelea na shughuli zake kila siku bila ya wasiwasi wowote’’,walieleza.

“Kila siku anakuja na magari ya maji pamoja na wafanya kazi wake na kuendeleza kilimo katika eneo hilo halafu sisi wanakijiji anatutolea maneno ya kejeli kwa kusema kuwa eti hatuna tunaloweza kumfanya kama tunapo pakwenda tukapeleke kesi zetu”.

Akizungumzia hali hiyo mwenyekiti wa kamati maalum inayohusika na usimamizi wa shirikishi wa rasilimali za ukanda wa pwani ICM ambayo ndio hasa inayohusika na suala hilo Mussa Makame Bam, alikiri kuwa ni muda mrefu tangu pale walipolipeke suala hilo katika vyombo husika na hadi sasa hakuna jawabu yoyote waliyoipata kutoka huko.

Alipoulizwa kama anayo taarifa ya wananchi wake kutaka kumzuwia mtu huyo asiingie kijijini ili kushinikiza suala hilo, alijibu kuwa hajapata taarifa hizo na kama jambo hilo lipo basi wanakijjiji hao tayari wanaonesha kuchoshwa na ahadi hewa za viongozi wa ngazi za juu.

Alifafanua kuwa mara ya mwisho alipojaribu kufuatilia suala hilo alijibiwa kuwa tayari limeshafikishwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, hivyo ameomba kama ni kweli suala hilo limefikishwa huko basi kufanyiwa maamuzi haraka ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza hapo baadaye

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.