Habari za Punde

JAJI MKUU AAPISHWA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein leo amemuapisha Mhe. Jaji Omar Othman Makungu kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.


Hafla hiyo ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Miongoni mwa viongozi hao waliohudhuria ni Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Abubakar Khamis, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Abdalla Mwinyi, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji, Kaimu Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar George Kazi, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar, Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib na viongozi wengine wa serikali.

Kuapishwa kwa Jaji Omar Othman Makungu kunafuatia uteuzi wake alioteuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein hapo Mei 1, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa uteuzi huo ulianza rasmi Mei mosi mwaka huu.

Rais Dk. Shein amefanya uteuzi uteuzi huo kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 94(1) chaKatiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Mwezi uliopita Jaji Makungu aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Aidha, Aprili 5 mwaka huu, Rais Dk. Shein alimteuwa Jaji Makungu kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa mjibu wa kifungu cha 94(4) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Jaji Makungu anachukua nafasi hiyo baada ya Jaji Hamid Mahmoud kustaafu kazi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa mujibu wa Sheria.

Jaji Makungu ameshika nafasi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC).

Pamoja na nafasi hizo pia, Jaji Makungu aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Jaji Makungu aliwahi kuwa Mwanasheria wa Serikali katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi kirefu.

Rajab Mkasaba, Ikulu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.