Habari za Punde

MAKAMPUNI YA UTURUKI KUWEKEZA ZANZIBAR - DK SHEIN

Na Nafisa Madai,MAELEZO Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein amesema Makampuni makubwa nchini Uturuki yatawekeza katika miradi mbalimbali Visiwani Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari jana usiku, Dk Shein alisema “ Tumezungumza na Wafanyabiashara wakubwa Uturuki na kwa kiasi kikubwa wamekubali kuwekeza, ingawa kwa sasa ni mapema kutaja thamani ya uwekezaji huo”

Rais Dk Shein alisema viwanja vya ndege, kile cha Karume Kisiwani Pemba kitajengwa na kuwa cha kisasa wakati Unguja, uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume nao utanufaika kwa kujengwa uzio.

Dk Shein alisema kwa sasa Serikali imo katika hatua za mwisho za kuifanyia marekebisho Mamlaka ya uwanja wa ndege kwa kutungwa sheria inayokidhi matakwa ya sasa nay a baadaye kwa kuanzisha Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar.

Alisema tayari Zanzibar na Uturuki, zimetiliana saini makubaliano ya awali kuhusu utafiti wa maeneo ya Uwekezaji ambapo utekelezaji wake umepangwa kuanza hivi karibuni.

Dk Shein amesema mbali na uwekezaji huo, pia sekta ya kilimo nayo imepewa msukumo kwa kukijengea uwezo Chuo cha Kilimo Kizimbani ikiwa pamoja na kuendeleza tafiti mbalimbali za kilimo.

Akizungumzia sekta ya elimu, Dk Shein amesema Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar kitakuwa na ushirikiano wa karibu na Chuo Kikuu cha Istanbul ikiwa pamoja na Wahadhiri kutoka Uturuki kutoa mihadhara ya kitaaluma SUZA.

Pia, idadi ya nafasi za masomo katika Tasnia ya Udaktari inatarajiwa kuongezeka kwa vijana kutoka Zanzibar kwenda kujifunza katika viwango vya Shahada ya Uzamivu, Shahada ya Uzamili na Stashahada ya juu ya Uzamili.

Dk Shein alisisitiza umakini kwa Watendaji wa Serikali katika kusimamia utekelezaji wa masuala hayo ambapo kabla ya kurudi Zanzibar, alifanya kikao na wasaidizi wake akiwataka kuhakikisha wanasimamia yale yote yaliyokubaliwa kwa wakati.

“Tumeanzisha dawati la kufuatilia ziara za Viongozi nje ya nchi, tumeanza na ziara ya Makamu wa Pili wa Rais kule Ushelishe, ziara ya Makamu wa kwanza wa Rais Falme za Kiarabu…naamini wanazifanyia kazi” Alisema Dk Shein.

Awali, Dk Shein alisema katika mazungumzo yake na Rais wa Uturuki, Abdullah Gul alimuomba kuwatoa wasiwasi Wafanyabiashara wan chi yake juu ya suala zima la amani na utulivu, ambapo Rais Dk Shein amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Zanzibar ni salama.

“Katika mazungumzo na Rais Gul, aliniomba nitakapokutana na Wafanyabiashara wa Uturuki niwaeleze suala la amani na utulivu, nimewatoa hofu na kwa bahati nzuri baadho yao wamekuwa wakija kimya kimya kutembea wamejionea hali ya utulivu na amani” Aliongeza.

Wiki iliyopita, Rais Dk Shein alifanya ziara rasmi ya Kiserikali nchini Uturuki ikiwa ni mwaliko wa Rais wa nchi hiyo. Zanzibar na Uturiki ina uhusiano wa muda mrefu tangu karne ya 16 A.D.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.