Habari za Punde

MATAIFA TAJIRI YAKWAMUE NCHI MASIKINI

Na Mwandishi Maalum, Istanbul

MAKAMU wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, ametoa wito kwa nchi tajiri kuzikwamua nchi maskini ili ziweze kukuza uchumi wake na kuwasaidia wananchi waliomo katika nchi hizo.

Dk. Bilal ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa unaojadili maendeleo ya nchi maskini unaofanyika nchini Uturuki.

Makamu wa Rais alisema mataifa maskini yametekeleza mambo mbalimbali ambayo yamesahauliwa na mataifa makubwa sambamba na mashirika ya kimataifa, huku kikwazo kikiwa kimebakia kwa mataifa makubwa kutimiza ahadi zao ili kuzikwamua nchi maskini.

“Kama ambavyo ripoti mbalimbali zinavyoonyesha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2001-2010, nchi maskini zimemudu kutimiza malengo yao mengi, kama sio makubaliano yote yaliyotolewa na nchi tajiri kwa nchi maskini. Jambo linalokatisha tamaa ni hali ya nchi tajiri kutotimiza ahadi wanazotoa”, alisema Dk. Bilal.

Akiipigia mfano Tanzania, Dk. Bilal alizielezea nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa, tangu kupitishwa kwa Azimio la Brussels mwaka 2001, Tanzania ilibadili sera zake nyingi zikiwemo zile zilizolenga kupunguza umaskini nchini kama MKUKUTA, ikaweka vyombo vya kusimamia ukuzaji wa uchumi, ikaongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya maamuzi, ikaainisha chombo cha kupambana na rushwa huku pia ikitoa uhuru mkubwa kwa vyombo vya habari.

Dk. Bilal alifafanua kuwa, Tanzania katika kipindi hicho imeongeza uwazi katika mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali, imefanikiwa kupitia upya mikataba ya madini na imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kutumia uwezo wake wa ndani kutanua wigo wa demokrasia nchini.

“Bado ipo haja kwa nchi maskini kupewa fursa zaidi katika soko ambalo halina masharti magumu. Kama hoja hii ikitekelezwa vyema ni wazi nchi hizi zitamudu ushindani katika biashara za ndani na zile za kimataifa. Hali iliyopo sasa haitoi fursa hizo,” alisema.

“Ili nchi maskini zimudu kuondoka katika kundi hili ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo, jukumu lililo mbele yetu ni moja ambalo ni kuweka mikakati ya wazi na kila upande kutimiza wajibu wake kama ambavyo Tanzania imedhamiria kufanya.”

Mifano mbalimbali ya Dk. Bilal aliyokuwa akiitoa katika hotuba yake ililenga kuonesha nafasi ya nchi maskini katika kujikwamua lakini akasisitiza kuwa jitihada hizo peke yake hazitoshi kwa kuwa nchi tajiri ndizo zinazodhibiti uchumi wa dunia, huku pia zikiwa na fursa nyingi katika ushindani kuliko nchi maskini.

Dk. Bilal yuko jijini Istanbul akiongoza ujumbe wa Tanzania unaohusisha pia wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia sambamba na wafanyabiashara.

Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuhusisha wabunge, wawakilishi wa asasi za kiraia na wafanyabiashara katika mkutano wake wa kujadili maendeleo ya nchi maskini tangu kuanza kwa mikutano hii miaka 30 iliyopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.