Habari za Punde

MGOGORO WA ARDHI WAFUMUKA BWELEO

Na Haroub Hussein

SHEHA wa Shehiya ya Bweleo, Haruna Migoda Mataka ameazimia kuwafikisha mahakamani wananchi wa Shehia hiyo walioamua kuvamia na kujimilikisha eneo la ardhi kinyume na sheria.

Kwa mujibu wa Sheha huyo wapo baadhi ya wananchi waliovamia eneo la ardhi linalojulikana kwa jina la kwa Laka, ambalo alidai kuwa ni la muwekezaji.

Akizungumza na gazeti hili, Sheha huyo alisema tayari wameshawasilisha malalamiko ya uvamizi huo wa ardhi katika kituo cha Polisi cha Mazizini, huku akitaka kuendelea na hatua zaidi za kisheria.

Alisema serikali ya kijiji chake ilishatoa uamuzi kuwa eneo hilo apewe muwekezaji na taratibu zote zilifuatwa katika kumpatia eneo hilo, ambalo hivi sasa baadhi ya wanakijiji wameamua kuupinga uamuzi huo.

“Kijiji tumeshakubaliana eneo la kwa Laka tumpe muwekezaji, tunashangaa kujitokeza baadhi ya wananchi kulivamia na kupimiana viwanja vya kujenga nyumba za makaazi”, alisema Sheha huyo.

Sheha huyo alipoulizwa ni muwekezaji gani aliyepewa eneo hilo na ni wa nje au wa ndani, alisema aliyepewa ni muwekezaji wa ndani na ni mzaliwa wa Zanzibar hata hivyo alishindwa kubainisha jina lake, huku akisisitiza kuwa taratibu za kumpa muekezaji huyo zilifuatwa.

Sheha huyo aliwatupia lawama wazaliwa wa Bweleo walioko mjini kuwa ndio waliopinga uamuzi huo, huku akisisitiza kuwa hawana haki kwani hawaishi katika kijiji hicho.

Sheha Migoda alisema kuwa tayari ameshafungua kesi katika kituo cha Polisi Mazizini pamoja na kuwajuilisha Idara ya Ardhi juu ya uvamizi huo uliofanywa na baadhi ya wananchi hao.

Kwa upande wao wananchi wanaodaiwa kuvamia na kujimilikisha eneo hilo walisema wameufurahia uamuzi wa kushitakiwa kwani wanaamini haki yao wataipata kupitia vyombo vya kisheria baada ya kuikosa katika vikao kati ya uongozi wa kijiji na wanakijiji.

Katibu wa kamati ya maendeleo ya kijiji cha Bweleo, Mataka Makame Mataka alisema wamechoshwa na vitendo vya kuchukuliwa ardhi yao na kupewa wageni huku wazaliwa wakikabiliwa na tatizo la ardhi ya makazi, kilimo na mifugo.

Katibu huyo alisema imekua ni kawaida kwa viongozi wa kijiji hicho kugawa ardhi kiholela kwa wageni huku ikisingizia kuwa ni wawekezaji jambo linalosababisha wanakijiji kubakia wakiwa hawana sehemu ya makazi.

"Sisi kamati ya maendeleo tulipeleka barua Idara ya ardhi tangu mwaka 2003 ya kuwaeleza kuwa kijiji chetu kimekuwa, hivyo watufanyie utaratibu wa kuja kutupimia eneo jengine ili tuweze kujenga nyumba za makazi hadi leo hatujajibiwa, lakini serikali ya kijiji imempa mtu wao wanayemwita muwekezaji eneo ili afanye shughuli zake sisi hatukubali tuko tayari tufunge sote lakini ardhi yetu tutaipigania hadi hatua ya mwisho", alisema katibu huyo kwa jazba.

Aidha alisema tayari wameshaandaa mpango wa kumuona Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ili aweze kuwasaidia katika kuwapatia haki yao wanakijiji hao ambayo ilichukuliwa kwa hadaa.

Alisema watahakikisha kuwa hakuna muwekezaji yoyote yule atakayewekeza kijijini hapo kwa sasa hadi hapo madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi kutoka kwa Balozi Seif ambaye ndie mtendaji mkuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Tunahakikisha hapa hawekezi mtu hadi Balozi atoe maamuzi tena tunamuomba aje aangalie mwenyewe hali halisi inayofanywa na viongozi wetu wa shehia na Wadi kwa kushirikiana na Matajiri hao, wanavyoimaliza ardhi ya kijiji hiki "alisema katibu huyo wa kamati ya maendeleo.

Mwandishi wa habari hii alipowatafuta watu wa Bweleo wanaoishi mjini kuzungumzia suala hili, walisema kuwa ni kweli kadhia hiyo ipo na hawakubaliani na maneno ya viongozi wao kuwa hawana haki katika kijiji hicho kwa vile hawaishi huko.

Alisema walilivamia siku ya Mei Mosi kwani ni siku ya kujikomboa kwa wafanyakazi nao wameamua kuitumia siku hiyo kujikomboa dhidi ya unyang'anyi huo wa ardhi waliyoirithi kutoka kwa wazee wao.

"Viongozi wetu hawatutendei haki sisi tuliopo mjini wakati wanapokuja watu na kutaka ardhi kijiji kwetu, hawaitishi mkutano wa wana Bweleo wote, bali huwaita wachache tena wale wasiojua hata wanasaini nini ndani ya karatasi ni sawa na mikataba ya machifu wetu wa wakati ule wa ukoloni wanasaini mikataba imeandikwa vyengine na wao wanaambiwa vengine", alisema mmoja wa wanakijiji wa Bweleo anayeishi mjini.

Aidha alisema wakati wa michango kwa ajili ya maendeleo ya wana Bweleo watu wote hata wale waliomjini lakini iweje wasishirikishwe kwenye suala la ardhi, alihoji mwananchi huyo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.