Na Salum Vuai, Maelezo
IDARA ya Mazingira Zanzibar iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, imekiri kuwa sheria inayopiga marufuku uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini ni dhaifu.
Ofisa wa maliasili katika Idara hiyo, Sihaba Haji Vuai, amewaambia waandishi wa habari kuwa, kutokana na kubainika mapungufu mbalimbali, sheria hiyo imefanyiwa marekebisho ili iweze kukidhi haja na kuondoa kero ya mifuko hiyo nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi kuhusu maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayofikia kilele Juni 5, Vuai alisema Idara yake inakabiliwa na changamoto kubwa katika kupiga vita uingizaji wa mifuko hiyo, ambayo imeendeelea kuonekana licha ya kupigwa marufuku.
Alieleza kuwa mapungufu ya sheria yalibainika baada ya Idara hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya dola kukamata jahazi iliyokuwa na tani 600 za shehena ya mifuko katika maeneo ya kisiwa cha Bawe wiki kadhaa zilizopita.
Ofisa huyo alifahamisha kuwa dhamira ya kuwafungulia mashitaka waliokamatwa na shehena hiyo liligonga ukuta baada ya ofisi ya Mwendesha Mashitaka kudai kuwa haoni kesi kutokana na sheria hiyo kutoonesha eneo ambalo linahakikisha kuwa watuhumiwa walikuwa na kesi ya kujibu.
Vuai alisema ni udhaifu uliomo kwenye sheria hiyo ni pamoja na kutokuwa na ushahidi wa kimaandishi unaonesha kituo ambacho mtuhumiwa alikuwa akipeleka mifuko hiyo kama sheria za kimataifa zinavyoelekeza.
Aidha, kwa kuwa mashua iliyobeba shehena ya mifuko hiyo haikukamatwa katika bandari ya Zanzibar ikiteremsha bali ilishikwa ikiwa safarini, ambapo watuhumiwa walisema walikuwa wakitokea Mombasa kwenda Kilwa, alisema hakukuwa na namna ya kuwafungulia kesi.
Pamoja na sababu hizo, lakini pia alisema kipengele cha adhabu kwa wanaopatikana na mifuko hiyo hakioneshi kuzingatia haki za binadamu kulingana na uzito wa makosa yenyewe, bali kinaonesha kuwakomoa wanaokamatwa.
Akifafanua, alisema kwa mujibu wa Ofisi ya DPP, haijuzu kumpiga faini ya shilingi milioni moja mtu anayeshikwa akiwa na mfuko wa robo kilo ya sukari ambao ameupata dukani, akisema hatua hiyo inaonesha ukandamizaji.
Kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ambayo alisema yako katika hatua za mwisho, adhabu kwa watakaopatikana na mifuko hiyo itaanzia shilingi 30,000 kulingana na uzito wa makosa ambao utaangalia kiasi cha mifuko itakayokamatwa pamoja na mambo mengine.
Hata hivyo, alisema marekebisho hayo hayatafuta adhabu ya kifungo cha miezi sita jela kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kuingiza au kutumia mifuko hiyo inayotajwa kuwa ni miongoni mwa sababu kubwa za uchafuzi wa mazingira nchini.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira hapa nchini yamepangwa kuanza Juni mosi kwa shughuli mbalimbali, na kufikia kilele Juni 5, kwa sherehe zitakazofanyika hoteli ya Bwawani.
No comments:
Post a Comment