Habari za Punde

WAWAKILISHI WAPINGA UCHIMBAJI MATOFALI PEMBA

Na Mwanajuma Abdi

SERIKALI imeshauriwa kuzuia ukataji wa matofali katika kisiwa cha Pemba hadi hapo patakapotolewa muongozo wa kutayarishwa kanuni za udhibiti na utunzaji wa mazingira kutokana kujitokeza uharibifu mkubwa.

Ushauri huo umetolewa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa juu ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi wa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012,  Mwanajuma Faki Mdachi wakati akichangia katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja.

Alisema ni vyema Serikali ikazuia ukataji huo ili kudhibiti uharibifu wa mazingira usiendelee Pemba kunakosababishwa na ukataji wa matofali, ambapo aliwashutumu viongozi na wanasiasa  wanachangia katika kadhia hiyo.

“Sisi viongozi wanasiasa tunachangia eti vijana watafanya kazi gani hapa duniani kuna kazi nyingi za kufanya ambapo mtu atapata riziki bila ya kuhifadhi mazingira ambayo huko mbele wakeshaacha mashimo makubwa na ardhi ikiwa haifai tena, vizazi vijavyo wataishi vipi na kama wazee wao walikata miamba kukawa na mashimo kama wanavyoyaacha hivi sasa wao wangeliridhika”, alihoji Mwanajuma Mdachi.

Aidha alitaka Wizara ya Miundombinu waache tabia ya kuchimba vifusi kwa miradi ya ujenzi wa barabara hasa inayofanywa na wafadhili bila ya kushauriana na kupata miongozo kutoka Idara ya mazingira ambapo wajenzi wakeshaondoka huacha mashimo makubwa, jambo ambalo huifanya
ardhi isiweze kutumika tena.

Alieleza licha ya uchimbaji huo unaelekeza kulipwa kodi kwa asilimia 10 katika Idara ya Mazingira lakini fedha hizo hazilipwi, ambapo uharibifu unapotokea kunakuwa hakuna nyezo za kuweza kurejesha hali hiyo.

Makamu Mwenyekiti huyo, alishauri Idara kuainisha maeneo ya vianzio vya maji ili kuvihifadhi visikatwe miti na kutoa muongozo wa upandaji wa miti inayosaidia kuongeza maji ardhini ili kuzifanya chemchem ziendelee kutoa maji kwa wingi na kwa muda mrefu bila ya kukauka.

Alifahamisha kuwa, jamii ikatae matumizi ya mifuko ya plastiki lakini pia jitihada za makusudi zinahitajika kuzuia uingizwaji wa mifuko hiyo nchini, ambapo jitihada kubwa zielekezwe katika kuifanyia marekebisho sheria ya utunzaji wa mazingira ambayo inaonekana kutoa mwanya kwa
waingizaji na watumiaji wa mifuko hiyo.

Aliongeza kwamba, baada ya marekebisho hayo utekelezaji wa sheria iweke bayana kwa yule atakayekwenda kinyume achukuliwe adhabu kali ili kukomesha vitendo hivyo.

Akichangia katika Idara ya Watu Wenye Ulemavu alisisitiza kutekelezwa kwa sheria ya ujenzi wa majengo rafiki kwa walemavu, kwani inaonekana dhahiri wajenzi wengi hususani majengo ya Serikali yanajengwa bila ya kuzingatia mahitaji ya walemavu hivyo atakwenda kinyume achukuliwe
hatua kali za kisheria.

Nae Mwakilishi wa Magomeni, Salmin Awadh akichangia katika bajeti hiyo, alisema uchafu wa mazingira uangaliwe upya kwa vile mji ni mchafu, ukianzia Mji Mkongwe na maeneo mbali mbali ya mji wa Zanzibar hali ambayo inaweza kuathiri mapato yanayotokana na utalii kutokana na
hali hiyo.

Hata hivyo, alipendekeza kupandishwa kwa miti kwa wingi katika kuleta haiba nzuri na uhifadhi wa mazingira Zanzibar katika kulinda rasilimali iliyopo.

Mwakilishi wa Mji Mkongwe Ismail Jussa alihoji fungu kubwa la fedha kwa Tume ya UKIMWI Zanzibar zilizotengewa ukiacha Idara nyengine ikiwemo ya dawa za kulevya.

Ali Waziri Fatma Fereji akija kufanya majumuisho amueleze fedha hizo zilizotengwa zitawanufaisha vitu watu wenye virusi vya UKIMWI, au zitatumika kwa semina ya mafunzo kwa watendaji na wengine wakijigawia mapesa, ambapo akitolea mfano wa Jumuiya ya ZAPHA+ katika bajeti hiyo
haikuanisha kwamba wanawasaidia vipi watu wanaoishi na VVU kwani wanaishia omba omba.

Mwakilishi Rashid Seif wa Ziwani, alisema nyumba za kurekebisha tabia ziongezwe kwani zinawasaidia vijana wanaoacha dawa za kulevya, sambamba na kuomba Serikali iwasaidia fedha nyumba hizo kwa vile zinajiendesha wenyewe, ambapo alihoji misaada mbali mbali ya wahisani
wanaoitoa hadi shilingi milioni 10 lakini aliuliza ni kweli zinawafikia walengwa isijekuwa watu wanagawana na zilizobaki kama 200,000 ndio zinapelekwa kwa walengwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.