Habari za Punde

KIKWAJUNI MENO NJE

Furaha yarindima wakongwe hao wakirudi ligi kuu

Na Mwajuma Juma
WAKONGWE wa soka visiwani humu timu ya Kikwajuni, wamefanikiwa kupanda daraja la ligi kuu msimu ujao baada ya kutoka sare na Mwenge ya Pemba kwa kufungana bao 1-1 kwenye dimba la Mao Dzedong juzi.

Kufuatia sare hiyo, Kikwajuni imerudi ligi kuu kwa ushindi wa jumla wa magoli 4-3, baada ya kushinda pambano la kwanza lililochzewa Pemba wiki mbili zilizopita.

Timu hizo zililazimika kucheza hatua hiyo kutokana na kushika nafasi za pili katika ligi daraja la kwanza taifa kanda za Pemba na Unguja.

Vijana wa ‘sauti ya tembo’, KISC, ndio waliotangulia kucheka na nyavu kwa bao la dakika ya 39 kupitia kwa mchezaji wake Abbas Abdallah.

Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko, na Mwenge waliokuwa wakihitaji ushindi wa angalau mabao 2-0, walikianza kipindi cha pili kwa kasi na mashambulizi ingawa walikumbana na ukuta mgumu wa Kikwajuni uliosimama imara kufagia hatari.

Hata hivyo, jitihada hizo zilizaa matunda katika dakika ya 80, pale Hussein Rashid alipoisawazishia timu yake kwa mkwaju wa penalti.

Matokeo hayo, yanakamilisha timu tatu zilizopanda ngazi hadi ligi kuu msimu ujao, ambapo Kikwajuni inaungana na timu ya Zimamoto kutoka Unguja na Super Falcon ya Pemba, ambazo zilishika nafasi za juu katika ligi daraja la kwanza taifa.

Aidha timu hizo zinakwenda kujumuika na  timu za Zanzibar Ocean View, Miembeni, Jamhuri, KMKM, Mafunzo, Polisi, Mundu, Chuoni na Chipukizi kucheza ligi kuu hiyo.

Wakati Kikwajuni ikifurahia mafanikio hayo, wakongwe wenzao Malindi wamejikuta wakiporomoshwa hadi daraja la kwanza baada ya miaka mingi ya kujitanafasi katia ligi kuu, ikiungana na  Duma na wanagenzi Madungu kushuka daraja.

Na katika ligi daraja la kwanza Taifa iliyomalizika wiki kadhaa zilizopita, maveterani Mlandege, Polisi Bridge na Kipanga wakatupwa chini hadi daraja pili  msimu ujao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.