Habari za Punde

MAALIM SEIF AKUTANA NA BALOZI MDOGO WA OMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sherif Hamad alipokuwa katika mazungumzo na Balozi mdogo wa Omananayemaliza muda wake  Majid Abdulla Al Abbad Ofisini kwake Migombani.

Na Abdi Shamnah –OMKR

 MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim seif Sharif Hamad amesema kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Oman umeimairika sana katika kipindi cha miaka sita, kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na Balozi mdogo wa nchi hiyo hapa nchini, Majid Abdulla Al –Abbad, ambae amemaliza muda wake.


Maalim Seif amesema hayo leo ofisini kwake Migombani alipokutana na Balozi huyo anaerudi nyumbani baada ya kuitumikia nchi yake kwa kipindi cha miaka sita.

Amesema Balozi Majid alikuwa mfano mzuri wa kukuza mashirikiano kati ya nchi mbili hizi, kutokana na juhudi zake binafsi za kusukuma mbele miradi kadhaa ya kijamii na kimaendeleo, ikiwemo uimarishaji wa Chuo cha Afya Mbweni.

Alisema pia atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa uliowezesha Serikali ya Oman kuliruhusu Shirika la Ndege la nchi hiyo ‘Oman Air’ kuanza tena safari zake kati ya Oman na Zanzibar, mbali na mapungufu yaliopo katika uwanja wa Ndege wa Zanzibar, hatua iliopunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la usafiri.

Alisema katika kipindi cha utumishi wake hapa nchini, Balozi Madjid alikuwa mtu wa karibu na wananchi, alieonyesha mshikamano na kushiriki katika shughuli mbali mbali za Kitaifa.

Maalim Seif alimshukuru Balozi huyo kwa kufanikisha ziara yake nchini Oman mapema mwaka huu, na kueleza imani ya Serikali ya Zanzibar juu ya utekelezaji wa masuala mbali mbali yaliokubaliwa.

Alisema Serikali ya Zanzibar, kwa msaada wa Oman, inaendelea na matayarisho ya kuandaa mkutano wa wafadhili (donars conference) utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Alimtakia maisha mema Balozi huyo na kuahidi kutoa kila aina ya ushirikiano kwa Balozi mwengine atakaekuja kuchukua nafasi yake.

Nae Balozi Madjid alisema Serikali ya Oman itaendeleza mahusiano na mashirikiano yake na Zanzibar, ili kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia juu ya ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais nchini Oman, Balozi Madjid alimhakikishia kiongozi huyo, kuwa mbali na kuchelewa  utekelezaji wa baadhi ya mambo yaliokubaliwa, kuna matarajiio makubwa ya kupatikana mafanikio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.