Habari za Punde

SENSA YA MAJARIBIO AGOSTI

Na Mwantanga Ame

WAZANZIBARI kote nchini wanatarajiwa kuanza kuhesabiwa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu katika zoezi la majaribio ili kuweza kujulikana idadi yao kamili.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Waziri huyo alisema serikali itaendesha zoezi hilo la sensa kwa ajili ya kuwahesabu Wazanzibari kote nchini ikiwa ni hatua ya kuweza kutambulika idadi yao.

Alisema sensa ya idadi ya watu itaweza kusaidia serikali kuipa fursa nzuri kuweza kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake.

Alisema wanalazimika kufanya sensa hiyo hivi sasa kutokana na kutimiza miaka 10 tangu kuendeshwa kwa zoezi na kuhesabu watu na makaazi mwaka 2002 jambo ambalo tayari kuna mabadiliko makubwa yanayohitaji kuangaliwa.

Alisema maandalizi ya sensa hiyo hivi sasa yapo katika hali nzuri chini ya usimamizi wa Mtakwimu Mkuu wa serikali Zanzibar na Tanzania Bara.

Kutokana na kuanza kukamilika matayarisho hayo Waziri aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa kukubali kuhesabiwa kwa kuwapa ushirikiano wataokuwa wanaifanya kazi hiyo ili lengo la serikali liweze kufanikiwa.

Alisema suala la ongezeko la idadi ya watu ni moja ya changamoto kubwa yenye uzito ambayo inahitaji kuangaliwa na pande zote za jamii ikiwa ni hatua itayoweza kupunguza tatizo hilo.

Waziri huyo alisema ili kupatikana mafanikio ni vyema wadau wote kuona umuhimu wa kutumia takwimu katika shughuli zao, ziwawezeshe kupanga mipango itayokuwa na usambazaji sawia wa raslimali huduma na miundombinu baina ya Mijini na Vijijini.

Alisema hali hiyo haitaweza kupunguza kasi ya vijana kukimbilia mijini bali itasaidia kupunguza dhana ya kwamba watu wa vijijini kulala mapema.

Kutokana na tafiti mbali mbali Waziri huyo alisema changamoto nyingi zinazohusu vizazi, vifo, uchafuzi wa mazingira na ujenzi holela ni mambo yenye uhusiano mkubwa na viwango vya elimu na hali ya utajiri au umasikini wa wananchi.

Hata hivyo Waziri alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema bado serikali itahakikisha juhudi za makusudi zinafanyika kupitia utekelezaji wa mpango wa MKUKUTA na MKUZA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.