Habari za Punde

UN HABITAT YAWAMWAGIA MIPIRA VIJANA ZANZIBAR

Na Khamis Akili, WUJMVWW
SHIRIKA la Makaazi Duniani (UN HABITAT) kupitia Mama Anna Tibaijuka, limekabidhi zawadi ya mipira 650 yenye thamani ya shilingi milioni saba, kwa timu za vijana za mikoa yote ya Zanzibar.


Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto Shangani mjini hapa.

Mkurugenzi wa Idara ya Vijana Mohammed Salim Ali, aliwakabidhi wawakilishi wa vijana wa mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini na Kaskazini Unguja kwa niaba ya Waziri Tibaijuka.

Mkurugenzi huyo aliwataka vijana nchini kuitumia michezo katika kuleta maendeleo na kukuza amani, kuimarisha umoja na kujiepusha na vitendo viovu katika jamii.

Aidha aliwakumbusha wawakilishi hao wa vijana wa mikoa wajibu wao wa kuwahamasisha vijana kupenda michezo kwa lengo la kuimairisha afya zao na elimu nchini.

Ofisa Michezo Wilaya ya Magharibi Hamad Omar Shehe, Ofisa Mipango Kusini Unguja Juma H. Juma pamoja na Ofisa Mipango Wilaya ya Kaskazini A Faida Salmin Juma, wakipokea mipira hiyo, walimshukuru Mama Tibaijuka na Serikali ya Zanzibar.

Walisema, taasisi hizo zimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo ya vijana  kupitia michezo na kuahidi kuifikisha mipira hiyo kwa wahusika ili kuinua viwango vya michezo kwa vijana nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.