Na Ramadhan Makame
MENEJA Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Hassan Ali Mbarouk amesema jenereta za kuzalishia umeme wa dharura zilizokuweko Motoni hazijasita kuzalisha nishati hiyo kutokana na ubovu.
Alisema jenereta hazo zimesita uzalishaji wa umeme kutokana na gharama kubwa za uendeshaji unaotokana na ughali wa mafuta ya dizeli yanayotumika.
Meneja Mbarouk alieleza hayo jana ukumbi wa shirika hilo uliopo Gulioni mjini hapa, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mambo mbali mbali kwenye mazungumzo na waandishi wa habari.
Alisema kuanzia mwezi Agosti mwaka jana hadi Machi mwaka huu, jenereta hizo zimetumia zaidi ya shilingi milioni 900, fedha ambazo zimetoka ndani ya shirika hilo.
Akifafanua zaidi alisema uzalishaji wa umeme wa jenereta una gharama kubwa na umekuwa na gharama kubwa ambapo uniti moja hugharimu shilingi 394 huku wateja wakinunua kila uniti kwa shilingi 120.
Taarifa ya Meneja huyo imekuja kufuatia hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari (sio Zanzibar Leo) kueleza kuwa jenereta hizo zimesitisha uzalishaji wa umeme kutokana na kuharibika.
Meneja huyo alisema taarifa za kuharibika kwa jenereta hizo zimewashitua wafadhili waliosaidia ununuzi wa jenereta hizo ambapo nchi ya Sweden, ilituma ujumbe kutaka ufafanuzi wa ndani juu ya kuharibika kwa jenereta hizo.
“Jenereta zetu zote ni nzima hakuna hata moja iliyoharibika, hazizalishi umeme sio kwa sababu ya kuharibika, hazizalishi kutokana na gharama za uendeshaji wake ni mkubwa”, alisema Meneja huyo.
Alisema jenereta hizo ambazo hutumia dizeli yenye madini kidogo ya salfa, hutumia lita 8,000 kwa siku ambapo kwa mwezi shirika hutumia kiasi cha shilingi milioni 280 kwa uendeshaji.
Jenereta hizo zilikuwa zikitumika kusaidia uzalishaji wa umeme ili kuupunguzia mzigo waya wa umeme wa chini ya bahari uliotoka jijini Dar es Salaam ambapo hivi sasa una uwezo wa kuleta megawati 40 huku mahitaji yakiwa ni megawati 55.
Akizungumzia kukatika kwa umeme katika nyakati za jioni alisema kunatokana na mitambo iliyoko jijini Dar es Salaam ambayo hushindwa kuzalisha umeme.
Meneja huyo aliwaomba wananchi kujitahidi kutumia vyema umeme kwani katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani matumizi huwa makubwa.
No comments:
Post a Comment