Na Halima Abdalla
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Mwinyihaji Makame amesema ziara zinazofanywa na viongozi wakuu wa Serikali zinazofanywa nchi mbali mbali zimekuwa na mafanikio makubwa kwa upande wa Zanzibar.
Alitoa mfano wa ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein nchini Uturuki, makubaliano kadhaa yamefikiwa ambapo Uturuki itashirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta za afya, utalii, elimu na kilimo.
Dk.Mwinyihaji alisema hayo alipokuwa akijibu suali la Hija Hassan Hija (Kiwani), aliyetaka kufahamu viongozi wa wakuu wa Serikali wanapofanya ziara nje, mafanikio gani yanayopatikana ambayo viongozi wetu wanatuletea.
Aidha alisema ushirikiano katika sekta ya afya utajumuisha kupatiwa wataalamu wa afya kutoka Uturuki kuja kufanya tathmini ya mahitaji katika Wizara ya afya, kuongezwa nafasi za masomo ya udaktari, dawa, ufundi, teknolojia ya habari na kupatiwa wataalamu watakaosaidia katika vitengo vya orthopaedic surgeon, cardiologists, pediatricians.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa utaratibu mzuri wa kufuatilia ahadi wanazopewa viongozi wanapotembelea nchi za nje, kwa kuweka maafisa maalum wa kuratibu, kusimamia na kufuatilia ziara za Serikali zinazofanywa na viongozi na ahadi wanazopewa wakati wa ziara hizo.
Maafisa hao wanatekeleza majukumu yao chini ya uongozi wa makatibu wakuu wa ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na mipango ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment