Habari za Punde

DCMA KUTOA STASHAHADA YA MUZIKI

Na Aboud Mahmoud

CHUO cha Muziki wa Nchi za Jahazi (DCMA) kikishirikiana na Idara ya Sanaa na Maonyesho ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kina mpango wa kuboresha stashahada ya muziki inayotolewa chuoni hapo ifikapo mwezi Septemba.


Viongozi wa chuo hicho Adel Dabo na Mohammed Matona, wameliambia gazeti hili kuwa, hatua hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi wa muziki wanaojifunza chuoni hapo, ili watambulike katika ngazi ya kimataifa.

Wamesema kutokana na mpango huo, wanafunzi watakaojiunga na chuo hicho kwa ajili ya masomo ya stashahada, watasoma kwa kipindi cha miaka miwili.

Waliwataja wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam watakaoshirikiana na DCMA, kuwa ni Profesa Mitchel Strumpf na Dk. Makoye.

"DCMA imejipanga kikamilifu katika utaratibu huo, mara wanapomaliza ngazi ya cheti, wanafunzi wetu wataingia hatua ya diploma kwa miaka miwili, hii itawasaidia kutambulika duniani kote kimuziki", alisema Adel Dabo.

Viongozi hao wamesema, lengo la DCMA ni kumuandaa msanii aweze kufikia kiwango cha juu katika fani hiyo, na hivyo kuweza kuendesha maisha yake kutokana na sanaa.

Wamefahamisha kuwa, maboresho hayo yamelenga katika mafunzo ya nadharia, uwezo wa kiteknolojia, biashara ya muziki na historia yake katika nchi za Kiarabu, Magharibi pamoja na muziki wa Kiafrika.

DCMA ni chuo pekee hapa Zanzibar kinachotambulika kufundisha sanaa ya muziki, ambapo pia kimewasaidia wasanii wengi ambao sasa wamekuwa mahiri katika fani hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.