Na Rajab Mkasaba
DIRA ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ni kuwa na jamii ya Wazanzibari wanaoishi katika mazingira mazuri, waliosalimika na Ukimwi na dawa za kulevya na wanao furahia haki na fursa kwa maendeleo mazuri ya kiuchumi.
Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais uliyasema hayo katika kikao maalum na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein katika muendelezo wa kukutana na Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia mpango kazi wa Wizara na uhusiano wa MKUZA na Dira ya 2020.
Katika Kikao hicho Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Idd na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Dr. Abdulhamid Yahya Mzee walihudhuria.
Ukieleza mikakati iliyojiwekea, ofisi hiyo ikiwemo ile ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2011/2012,ukiongozwa na Waziri wake, Mhe. Fatma Ferej ulieleza kuwa katika kufikia Dira hiyo, afisi hiyo itaratibu na kutoa miongozo na kuweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria ili kurahisisha utetezi na uhamasishaji wa mambo yanayohusiana na Ukimwi, Mazingira, Dawa za Kulevya na Watu Wenye Ulemavu.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa miongoni mwa malengo waliyojiwekea kufikia malengo ya MKUZA ambayo yatapelekea kufikia malengo ya Dira 2020 na hatimae kuchangia katika kufikia malengo ya Milenia ni pamoja na ina kuweka mfumo endelevu wa usimamizi wa mazingira na kutekelezwa kwa mpango mkuu wa usimamizi wa taka.
Jengine ni kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na kuhakikisha waajiri wanatekeleza mahitaji juu ya haki zinazolenga kuleta usawa wa kijinsia na fursa sawa kwa watu wenye ulemavu pamoja na makundi mengine maalum na mwitikio wa mapambano dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.
Pamoja na mambo mengineyo Afisi hiyo ilieleza malengo mengine ni kuinua kiwango cha usalama na uhifadhi wa ustawi wa jamii kwa wasiojiweza na wale walio katika makundi maalum, kutoa huduma kwa watu wenye matatizo ya kiafya ya muda mrefu pamoja na kukuza utoaji wa huduma maalum.
Wakati huo huo Dk. Shein alifanya mkutano na uongozi wa Afis ya Makamu wa Pili wa Rais ukiongozwa na Waziri wake Mhe.Mohamed Aboud ambayo ilieleza Mpango Kazi wake kwa mwaka 2011/2012 na kueleza kuwa hivi sasa Zanzibar ipo katika utulivu mkubwa na umoja ambao chanzo chake kinatokana na maridhiano yaliyofikiwa na vyama vya CCM na CUF.
Afisi hiyo ilieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Saba imejenga mazingira mazuri ya mashirikiano baina ya viongozi na wananchi na kila mmoja kuweka mbele maslahi ya Taifa jambo ambalo limewezesha kufanyakazi kwa pamoja.
Ilieleza kuwa jitihada hizo zimepongwezwa na Jumuiya za Kimataifa na Washirika wa Maendeleo na kusisitiza haja ya kuendelezwa kwa juhudi hizo.
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais ileielza kuwa wananchi na ulimwengu wote kwa jumla umeshuhudia namna Zanzibar inavyojiimarisha kidemokrasia ushahidi ambao unapatikana kwa namna mijadala ndani ya Baraza la Wawakilishi jinsi waheshimiwa Wajumbe walivyoihoji serikali na serikali ilivyojibu kwa nia ya kuleta maslahi ya wananchi.
Aidha, afisi hiyo ilieleza kuwa Tume ya Uchaguzi imeendelea na jitihada zake za kuimarisha utendaji bora wa Tume pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika wakati wa Uchaguzi Mkuu na kabla ya hapo, ili kujenga mazingira mazuri kwa chaguzi zinazokuja.
Pamoja na hayo, afisi hiyo ilieleza miongoni mwa malengo yake ikiwa ni pamoja na kupunguza umasikini wa kipato kupitia miradi ya wananchi, kuweka mazingira ya kuwezesha ukuaji wa uchumi pamoja na kuimarisha demokrasia na Umoja wa Kitaifa.
Afisi pia, ilieleza lengo lake la kutayarisha na kutekeleza mkakati wa kukabiliana na maafa, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni na historia ya nchi pamoja na kuongeza ushirikishwaji wa jamii katika utawala wa kidemokrasia na upatikanaji wa taarifa na mengineyo.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi zake kwa uongozi wa Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ukiwemo uongozi wa Juu na kumpongeza Maalim Seif Sharif pamoja na Waziri wa Wizara hiyo kwa kusimamia vizuri Wizara hiyo pamoja na watendaji wake akiwemo Katibu Mkuu kwa juhudi zao licha ya uchanga wa Afisi hiyo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ukiwemo uongozi wa Juu na kumpongeza Balozi Seif Ali Idd pamoja na Waziri wake kwa kusimamia vizuri Wizara hiyo na kutoa pongezi kwa watendaji wake akiwemo Katibu Mkuu kwa hatua nzuri waliofikia.
No comments:
Post a Comment