Na Haji Nassor, ZJMMC
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kuwa umoja na mshikamano unaooneshwa na waumini wa dini ya kiislamu nchini kwa kujumuika pamoja kwenye futari, ni vyema ukaendelezwa kwenye shughuli nyengine za kimaendeleo.
Alisema kutokana na kuwa umoja ndio ngao ya kufakinikisha kila jambo, hivyo ni vyema ukaendelezwa na kushiriki hata katika masuala ya kimaendeleo, ili taifa lipige hatua kubwa ya mafanikio.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, kwa niaba yake, huko hoteli ya Clove Inn mjini Chake Chake, alipokuwa akizungumza na waumini ya dini ya kiislamu mara baada ya futari ya pamoja.
Dk. Jakaya alisema kuwa, kila jambo linaweza kufakiniwa pindi nguvu ya pamoja na mshikamano itaendelezwa katika kufakinikisha miradi mbali mbali ya kimaendeleo katika jamii.
“Ndugu waislamu nawashukuru kwa kuonesha umoja na mshikamano wenu huu wa kuhudhuria kwa wingi katika futari, lakini pia mjaribu kwa umoja kama huu, pia kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo”, alisema Dk.Kikwete.
Mapema Sheikh Jamal Abdallah Abedi, alisema suala la kufutarisha ni miongoni mwa sadaka bora mbele ya Mwenyezi Mungu ambapo pindi mfutarishaji akifariki malipo yake huendelea.
Alieleza kuwa ni vyema kila mmoja kwa mujibu wa nafasi yake akafanya hivyo, ili kujipatia neema zisizo na idadi kutoka Mwenyezi Mungu, kwani sio busara kwa muislamu kudhamini mambo zaidi ya kidunia na kuacha kutengeneza akhera.
No comments:
Post a Comment