Habari za Punde

ZOEZI LA UNUNUZI LAENDELEA VIZURI


Makamu wa kwnaza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad akiangalia karafuu zilizochakachuliwa kwa pamoja na unga wa makonyo, mchanga na maji, katika Ghala la kuhifadhia karafuu Mkoani kisiwani Pemba.Kulia ni Meneja Mkuu wa ZSTC Hamad Khamis Hamad na kushoto ni Mkuu wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa.Picha na OMKR

Na Abdi Shamnah

IMEELEZWA kuwa zoezi la ununuzi wa karafuu katika Wilaya ya Mkoani msimu huu, limekuwa likiendelea kwa mafanikio makubwa, ambapo hadi kufikia Agosti 15, mwaka huu, jumla ya tani 124.8 zilikuwa tayari zimenunuliwa na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC).



Hayo yameelezwa na Naibu Meneja Mkuu wa ZSTC Hamad Khamis Khamis, kufuatia ziara ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad inayoendelea kisiwani Pemba, yenye lengo la kuangalia shughuli mbali mbali za uimarishaji na uokozi wa zao hilo msimu huu.

Katika ziara hiyo Maalim Seif alitembelea maeneo kadhaa ya Wilaya ya Mkoani na kutembelea shughuli mbali mbali, ikiwemo kuangalia vitalu vya miche,vituo vya ununuzi pamoja na ghala la kuhifadhia karafuu.

Amesema wakulima wamehamasika na kuitikia vyema wito wa Serikali wa kulihami zao hilo na kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa, ikiwemo ile ya kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC.

Alisema hali ya ununuzi wa karafuu inaendelea vyema, na kuainisha kuwa kwa asilimia 99 ya karafuu zote zinazonunuliwa ni zile za daraja la kwanza, hatua iliolifanya shirika hilo kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 1.72 hadi hivi sasa.

Hata hivyo Naibu Meneja huyo alisema mbali na mafanikio hayo, kumekuwapo na matukio ya udanganyifu yanayofanywa na baadhi ya wananchi kwa lengo la kujiongezea kipato isisvyo halali.
Alisema baadhi ya wakulima wasio waaminifu wamekuwa na tabia ya kusaga makonyo na kuyachanganya na karafuu safi, ili kuongeza kiwango cha karafuu zao, hatua inayosema inaweza kulitia shirika hasara kubwa.

Aidha alisema wako miongoni mwao wanaosaga makonyo na kuchanganya na mchanga pamoja na maji ili kuongeza uzito, huku wengine wakidiriki kuzikaanga karafuu mbichi katika magae.

Alieleza kuwa mbali na hatari iliopo ya kulitia hasara Shirika lake, lakini pia hatua hiyo inazipotezea sifa na ubora wa kiwango karafuu pale zitakapofikishwa katika soko.

Khamis alisema ukosefu wa sheria inayobainisha hatua za kuchukuliwa dhidi ya mtu atakaepatikana kuhusika na matukio ya aina hiyo ni moja ya changamoto kubwa inayolikabili Shirika katika kukabiliana na udanganyifu.

Katika hatua nyingine baadhi ya wananchi waliokuwa wakijishughulisha na kazi za kusafirisha zao hilo kwa nnjia ya magendo nje ya nchi, wameibuka na kuungama, huku wakiiomba Serikali kuwapatiwa mikopo ili waweze kuijiendesha kimaisha baada ya kustaafu kazi hiyo.

Mmoja wa wanamagendo hao wastaafu Mohammed Zubeir Suleiman wa Mjimbini alisema kuwa Serikali imefanya uamuzi wa busara kuongeza bei ya zao hilo, hivyo hawana sababu ya kuendelea na shughuli hiyo, lakini akasema wanalazimika kupata mikopo kwa vile hawana shughuli mbadala ya kuendeshea maisha yao.

Akitoa ufafanuzi wa ombi hilo, Afisa Mdhamini wa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko Pemba Hemed Suleiman Abdalla, alisema tayari Wizara imekaa kikao na kuwataka wanamagendo hao wastaafu kujikusanya kikundi na kujisajili ili waweze kusaidiwa kupitia miradi mbali mbali, huku akiweka wazi kuwa ni vigumu kumsaidia mtu mmoja mmoja.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akitoa tathmin fupi ya ziara hiyo, alilipongeza shirika la ZSTC , kupitia Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko kwa kuwa na mipango bora msimu huu ya kulihami zao la karafuu.

Alisema Serikali inaunga mkono dhamira za wakulima binafsi wenye azma ya kuanzisha vitalu vya miche ya mikarafuu kwa lengo la kongeza kasi ya kuliimarisha zao hilo, sambamba na kuwapongeza wananchi kwa kuitikia wito wa Serikali wa kuuza karafuu zao ZSTC.

Alitaka wananchi waendelee kuelimishwa umuhimu wa uhifadhi bora wa karafuu pamoja na kuzingatiwa umuhimu wa Polisi jamii kama njia ya kukabiliana na biashara ya magendo ya karafuu.

Aidha alilitaka Shirika la ZSTC kuendelea kuwahudumia wakulima wenye karafuu zilizo mbali na vutio vyua kuuzia kwa kuwapelekea magari ili kuwapunguzia tatizo la usafiri.

Maalim Seif alitumia fursa hiyo kuutahadharisha uongozi wa ZSTC kuwa makini katika mpango wake wa utoaji wa mikopo kwa wakulima, na kushauri kuwepo mikataba ilio wazi na yenye kuainisha adhabu kwa yyeote atakaekwenda kinyume na mikataba hiyo.

Aliwataka wajifunze kutokana na makosa yaliopita huko nyuma, ambapo Shirika hilo lilipata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 74 baada ya baadhi ya wadeni wake kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Katika ziara hiyo Maalim Seif alipata fursa ya kutembelea shamba la mkulima Salim Mohammed na Kitalu cha Serikali cha miche ya mikarafuu kiliopo Mkatamaini pamoja na Kambi ya karafuu Tangaani.

Aidha alitembelea kambi ya karafuu Kimbuni, kituo cha ununuzi wa karafuu Mjimbini pamoja na kukagua ghala la karafuu Mkoani.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.