Na Kunze Mswanyama, Dar
KURUGENZI ya Mawasiliano ya Ikulu, imekanusha taarifa zilizotolewa na aliyekuwa Balozi wa Marekani hapa nchini, Michael Retzer ambaye amedai kuwa aliandaliwa safari ya Uingereza na kununuliwa suti tano Rais Jakaya Kikwete.
Aidha Kurugenzi hiyo ilisema mbali ya madai hayo ya uongo yaliyotolewa na Balozi huyo alieleza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichangiwa shilingi bilioni 5 mwaka 2005 kwa ajili ya kampeni na mfanyabiashara Ali Albwardy.
Taarifa ya Kurugenzi hiyo imekuja kufuatia Balozi huyo kueleza katika ripoti zake ilizozituma nchini kwake na kudakwa na mtandao Wikileaks.
Katika ripoti ya Balozi huyo alisema gharama hizo zilitolewa na aliyekuwa mmiliki wa hoteli ya Kilimanjaro Kempiski raia wa Falme za Kiarabu, ambapo naye alitaka kusaidiwa kupatiwa kibali ili aweze kujenga hoteli zake kwenye mbuga za Serengeti na Ngorongoro.
Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, amesema madai hayo kwa mujibu wa Retzer yalitokana na mazungumzo kati yake na aliyekuwa Meneja na Mkurugenzi wa habari wa hoteli hiyo, Lisa Pile.
Alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati huo akiwa ni waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, hakuwahi na hatawahi kutumia mali za watu binafsi kwa maslahi yake kwa kuwa yeye kama waziri wa mambo ya nje hupatiwa posho kwa ajili ya mavazi yake kwa kuwa ndiyo kioo cha nchi yetu kimataifa.
"Rais amesikitishwa sana na madai haya, Kurugenzi inasema waziwazi kuwa hajawahi kuomba au kupokea zawadi yoyote toka kwa Ali Albward. Haya ni madai yasiyokuwa na ukweli wowote na kama kuna ushahidi wowote wa kuthibitisha madai haya basi utolewe hadharani hasa kuhusu lini na duka gani huko London, ili umma uweze kushuhudia ushahidi huo, vinginevyo madai haya yanabakia kuwa uongo tu".
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, hapajawahi kutokea wakati wowote,wakati Rais akiwa ni waziri wa Mambo ya Nje ama hata sasa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliposafirishwa na Ali bwardy au mtu yeyote kwenda London kwa ajili ya kununuliwa suti 5.
Kuhusu CCM kuchangiwa dola milioni moja (sawa na zaidi ya shilingi bilioni 5) kwa ajili ya kampeni ya chama hicho 2005, alisema Rais wakati huo alikuwa ni mgombea hivyo hawezi kabisa kuhusika na uombaji,ukusanyaji au uhifadhi wa michango hiyo pia kwenye orodha ya majina ya walioombwa kuchangia gharama hizo,Albwardy au hoteli yake hawamo.
Hata hivyo,taarifa hiyo inaonesha kuwa mfanyabiashara huyo hakuombwa au kuchangia hata senti moja kwa ajili ya harakati za uchaguzi huo mkuu na kuongeza kuwa,huku Salva akiongeza kuwa Rais Jakaya huvaa suti za bei ya kawaida tu na anapoonekana amependeza hiyo ni namna zinavyomkaa na siyo kwamba ni za gharama kubwa.
Msemaji huyo wa Ikulu alisema kuwa kama kweli angepokea zawadi hizo ingekuwa ni vigumu sana kukataza ujenzi wa hoteli hizo na hiyo inathibitisha kuwa rais hakupokea kitu chochote toka kwa mfanyabiashara huyo.
Alipoulizwa kama kuna hatua zozote za kisheria zitakazochukuliwa na serikali kwa kumdhalilisha mkuu huyo wa nchi,Salva alisema kuwa vyombo vingine vya serikali vinaangalia juu ya hatua zingine hivyo madai hayo yapo katika idara zinazohusika na mambo hayo.
Mtandao wa wikileaks, umejipatia umaarufu duniani hasa siku za hivi karibuni kwa kutoa siri kadhaa za mazungumzo yaliyofanywa na waliokuwa au viongozi mbalimbali wa serikali baada ya awali kutoa mazungumzo ya baina ya balozi mmoja wa Marekani na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Dk.Emanuel Hosea kuwa alimwambia balozi huyo kwamba, vita ya rushwa nchini inakumbatiwa na Rais Kikwete na kwamba ni ngumu sana kumalizika.
Hata hivyo siku chache zilizofuata, Dk.Hosea alikanusha na pia kuwaambia wananchi wasiamini maneno hayo kwa kuwa yalipopatikana hayakusemwa hadi alipomaliza muda wake hapa nchini na kuondoka na kwamba ni uongo tu.
No comments:
Post a Comment