BENKI ya KCB, inakusudia kuwasomesha watoto yatima waliotokana na ajali ya meli ya Mv. Spice Islander I, iliyopata ajali na kuzama usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita wakati ikitokea Unguja kuelekea kisiwani Pemba.
Mkurugenzi wa benki hiyo Rajab Ramia alieleza hayo alipokutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Balozi Seif Ali Iddi wakati benki hiyo ilipokwenda kutoa misaada kwa ajili ya waathirika wa janga hilo.
Mkurugenzi huyo alisema benki hiyo itawasomesha watoto yatima hayo ikiamini kuwa msaada huo ni umuhimu kwa maisha yao ya baadae na hasa ikikumbukwa kuwa hawakutarajia kuwapoteza wazee wao.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa benki hiyo itawasimamia yatima hao katika masomo yao kwa kuwapatia mahitaji na vifaa vya kielimu kama madaftari sare za skuli na vifaa nyengine wanavyohitaji.
Msaada mwengine ambao benki hiyo imejitolea ni kuona itawapatia watoto hao malipo ya ada kwa wanafunzi wanaotoka elimu ya msingi na kwenda sekondari.
Alisema wanachosubiri ni taarifa za wizara husika kuwapatia tathimini ya mahitaji na idadi ya watoto wanaohitaji msaada huo kwa wale ambao walipoteza wazee wao wote.
Alisema watoto hao wanahitaji misaada kwani wamekosa malezi ya familia na benki yao itakuwa tayari kuhakikisha wanabakia salama katika maisha yao na kusoma vizuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Balozi Seif Ali Iddi, alisema serikali imefarajika na msaaada huo kwa kuona watoto hao watakuwa katika hali nzuri ya kupata elimu yao.
Alisema mchango huo ni mkubwa na serikali inauthamini kwa hali ya juu kuona benki hiyo inavyowajali wananchi wa Zanzibar katika hali zote.
Balozi Seif, aliahidi kuhakishana inaipatia Benki hiyo majina ya watoto ambao watahitaji kupatia msaada ambapo Wizara yake itawasilisha majina hayo mapema kuanzia sasa.
Wakati huo huo Benki ya Exam Benki tawi la Zanzibar limejitolea lita 2000 za mafuta ya petroli kwa ajili ya kufanyika kwa doria kwa vyombo ambavyo serikali itavitumia kwa ajili ya kusaka watu ambao wanaodaiwa bado hawajapatikana.
Msaada huo umetolewa jana na Benki hiyo kwa Makamu wa Pili baada ya uongozi wa Benki hiyo kutoa ahadi hiyo mbele ya waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed huko Vuga Mjini Zanzibar.
Uongozi wa benki hiyo ulieleza juu ya kusikitishwa kwake na tukio hilo na kuiomba serikali na wananchi kuwa na moyo wa subira juu ya hali hiyo.
No comments:
Post a Comment