Na Mwandishi wetu
TUME ya Haki za Binaadam na Utawala Bora imesema ushuhuda uliotolewa na waathirika wa janga la ajali ya kuzama kwa Mv Spice Islander mwishoni mwa wiki iliyopita, umebainisha maofisa wa meli na baadhi ya taasisi zilichangia au hazikusaidia kueiepusha ajali hiyo.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kamishna wa Tume hiyo Zanzibar, Zahor Khamis, amesema kuzama kwa meli hiyo kumeanzisha masuali mengi likiwemo kwanini kampuni inayomiliki meli hiyo iliuza tiketi nyingi zaidi ya uwezo wa kubeba abiria.
Alisema ushuhuda huo wa waathirika unaibua masuali mengi yanayoonesha kuwa ama wapo maofisa na taasisi hazikuwajibika ipasavyo kuizuia ajali hiyo iliyogharimu maisha ya zaidi ya watu 190.
Mkurugenzi huyo alihoji kwanini kampuni inayomiliki meli hiyo iliuza tiketi za kubebea abiria kinyuma na uwezo iliyonao.
Aidha mbali na suali hilo, Tume hiyo ilihoji kwanini maofisa wa bandari na usalama waliiruhusu meli hiyo ipakie abiria zaidi ya uwezo wake.
Mkurugenzi huyo alisema Tume yake imepata mashaka kwanini meli hiyo iliruhusiwa kuondoka huku wakijua fika hakuna usalama wa abiria waliopakiwa.
“Taasisi zinazohusika na usalama wa vyombo vya majini na abiria vilikuwa wapi wakati wa kupakia abiria na kuridhia meli ianze safari”, aliieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, Zahor alishindwa kuamini kama nahodha wa meli hiyo na wasaidizi wake wanautaalamu wa kutosha katika kazi yao kwani hajui kitu kilichowaongoza hadi kujiirisha kuwepo usalama wa chombo chao na abiria.
Alisema kuwa ushuhuda uliotolewa na waathirika wa janga hilo umethibitisha kuwa maofisa wa meli na baadhi ya taasisi zilichangia au hazikusaidia kueiepusha ajali hiyo.
Tume hiyo ilisema kuwa mbali serikali kutangaza azma ya kuunda tume ya uchunguzi wa ajali hiyo, ilishauri kuwa iwepo mikakati itakayohakikisha hatua zinachukuliwa kuepusha ajali za namna hiyo.
Mkurugenzi huyo alitumia nafasi hiyo kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki waliokumbwa na msiba na kuwaomba wawe na subira katika kipindi hicho kigumu cha maombolezo.
Zahor alizipongeza juhudi za serikali zote mbili kwa kusaidia gharama za mazishi ya marehemu pamoja na kuwazika wale ambao hawakutambuliwa pamoja na serekali kubeba jukumu la kugharamia matibabu ya majeruhi.
No comments:
Post a Comment