Habari za Punde

MAMA WA KITALIANA ABAMBWA NA HEROIN

Na Ramadhan Himid, Polisi

KITENGO cha Kupambana na dawa za kulevya kilicho chini ya Makao Makuu ya Polisi Zanzibar kimefanikiwa kumkamata mama mmoja wa Kitaliano kwa tuhuma za kujishughulisha na biashara ya dawa za kulevya.


Akithibitisha kukamatwa kwa mama huyo rai wa Kitaliano, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi Muhudi Juma Mshihiri, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba 3 mwaka huu majira ya saa 9 Alasiri huko nyumbani kwake Vuga Mjini hapa.

Alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Giuliana Moschini Savano (46) Mtaliano wa Vuga Mjini Unguja kwa kukutwa na kete 303 aina ya ‘heroin’, ambazo zinasadikiwa ni dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi huyo inaaminika kuwa siku ya tukio mtuhumiwa aliweka kete hizo chini ya kitanda cha shemegi yake Mussa Bakar Hassan (28) ambae anaishi nae katika nyumba moja.

Taarifa pia kutoka raia wema zinasema kwamba mama huyo wa Kitaliano ni mtumiaji na mfanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kipindi kirefu kabla ya kukamatwa kwake.

Naibu Mkurugenzi huyo pia alisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema na hivyo kuwataka wananchi hao waendelee kutoa taarifa zao ili kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.

Mtuhumiwa huyo yupo mikononi mwa Polisi na kesi dhidi yake itasikilizwa Mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.