WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman amesema serikali haiko tayari kuona wafanyakazi wanadhalilishwa na waajiri.
Akitoa nasaha kwa wajumbe wa bodi ya ushauri wa mambo ya kazi baada ya kuizindua bodi hiyo, Haroun alisema kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya waajiri kuwanyanya wafanyakazi kwa sababu ambazo hazikubaliki.
Aidha aliapa kwenda nao sambamba waajiri wa aina hiyo mpaka pale watakapo acha tabia hiyo na kuwatendea haki wafanyakazi kwa mujibu wa sheria za kazi.
Alisema wizara imekuwa ikipokea malalamiko juu ya kuwepo kadhia hiyo na kuyashughulikia chini ya Kamisheni ya Kazi na Idara ya Ajira ambapo tayari imekutana na taasisi na hoteli zenye tabia hiyo na kuwataka ziache tabia hiyo mara moja.
Alisema wafanyakazi wa majumbani nao ni lazima wafanyekazi kwa utaratibu unaoeleweka ikiwemo kupatiwa mikataba ili waweze kupata haki zao kisheria.
Akizungumzia majukumu ya bodi hiyo ya ushauri wa masuala ya kazi, waziri Haroun alisema serikali inataka kuona washirika wote wa masula ya kazi waajiri, waajiriwa na serikali wanakuwa na kauli moja juu ya maslahi ya wafanyakazi na Taifa.
"Nnataka tuwe na kauli moja, sauti moja, lugha moja na msimamo mmoja juu ya maslahi ya wafanyakazi ili kuepusha malalamiko ya wafanyakazi na waajiri",alifafanua waziri Haroun.
Aliitaka bodi hiyo ambayo ina wajumbe 10, ikiwa na uwakilishi kutoka katika utatu, kufanya kazi kwa maelewano na kuishauri vyema serikali juu ya masuala ya kazi.
Nae Mwenyekiti wa bodi hiyo Ibrahim Mzee aliahidi bodi kufanyakazi kwa uadilifu, umakini, uaminifu na kwa ukweli katika kuishauri serikali juu ya masula ya kazi kwa maslahi ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo alisema kwa vile serikali kupitia kwa Waziri Haroun imewaamini kwa kuwachagua kwa shughuli hiyo hivyo ni wajibu kwa kuwa waamini kwa kazi hiyo na Taifa.
No comments:
Post a Comment