Na Mwinyi Sadallah
Meli ya Spice Islander iliyozama kisiwa cha Nungwi mapema wiki hii na kuua zaidi ya watu 200 imeripotiwa kuwa kwa mara ya mwisho ilifanyiwa ukaguzi Desemba, 2010, NIPASHE Jumapili imebaini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Visiwani Shipping Salum Said Mohammed ‘Batashi’ alisema meli hiyo ilikaguliwa baada ya kupelekwa Chelezoni Mombasa Kenya , Julai 20 hadi Agosti 8 mwaka 2010.
Meli hiyo ilitengenezwa Mwaka 1974 na Kampuni ya Gogumass Shipping yard ya nchini Uturuki ikiwa na uwezo wa kubeba tani 425 na abiria na 600.
Wakati ukaguzi ukitakiwa kufanyika kila baada ya miezi mitatu, Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wakaguzi wa meli zinazotoa huduma za usafiri wa abiria na mizigo katika mwambao wa bahari ya Tanzania.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umegundua uhaba huo umeanza kujitokeza tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kuamua kuanzisha Mamlaka yake ya kusimamia usafiri baharini, kazi ambazo zilikuwa zikifanywa na Mamlaka ya Usafirishaji nchi kavu na baharini (Sumatra) mwaka 2006.
Sumatra walitakiwa kuondoka Zanzibar baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (CUF) kulalamika kwamba mamlaka hiyo ilikuwa ikitoa huduma zake Zanzibar kinyume na sheria kwa sababu masuala ya usafiri baharini hayamo katika orodha ya mambo ya Muungano.
Uhaba huo wa wakaguzi wa meli umejitokeza huku kesi za vyombo vya usafiri baharini kuharibika injini zikiwa njiani na kusitisha safari zake, zikiendelea kujitokeza ambapo wiki hii boti mbili zimekatisha safari ikiwemo boti ya Sea bus I, ambayo ililazimika kurudi baandari ya mkoani Pemba baada ya injini moja kuzimika ilipokuwa ikielekea kisiwani Unguja na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa abiria.
Aidha boti ya Sea Star nayo ililazimika kukatisha safari na kurudi katika bandari ya Malindi Septemba 12, mwaka huu, baada ya injini moja kuharibika ilipofika katika kisiwa cha Chumbe ikielekea jijini Dar es Salaam. Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini mamlaka ya Usafirishaji Zanzibar ina wakaguzi wa meli wawili tu, wakati mahitaji yake ni wakaguzi sita, wawili Pemba na wanne Unguja.
Taarifa kutoka ndani ya Mamlaka hiyo imesema meli zilizosajiliwa Zanzibar mbali ya zile za kigeni zipo 80 zikiwemo meli za abiria 30 ambazo kwa mujibu wa sheria zinatakiwa kukaguliwa kila baada ya miezi mitatu.
Kutokana na tatizo hilo meli nyingi zinashindwa kukaguliwa kwa muda muafaka ikiwemo meli ya MV Spice Islanders iliyozama na kuua watu 204 na watu 619 kuokolewa, Septemba 10, mwaka huu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, Vuai Haji alikataa kuzungumzia mambo mbali mbali yaliyojitokeza tangu kutokea kwa ajali hiyo kwa madai kwamba msemnaji pekee ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed.
“Tumepokea maelekezo ya Serikali haturuhusiwi kuzungumza jambo lolote kuhusiana na meli na kazi hiyo kapewa waziri,” alisema.
Kwa mujibu wa Sheria kuweka utaratibu wa kusajili meli, usalama, na ulinzi na usafiri wa baharini ya mwaka 2006 imesema ni kosa kwa meli yoyote kwenda baharini na kutoa huduma kabla ya kupewa cheti maalumu.
“Meli yoyote ya Tanzania Zanzibar haitaruhusiwa kwenda baharini isipokuwa iwe imekaguliwa na kupewa vyeti maaalum,” kinaeleza kifungu cha 209 (1).
Aidha, sheria hiyo imeeleza iwapo meli itatoa huduma bila ya kuzingatia kifungu hicho, Mmiliki na nahodha ni wakosa na kila mmoja akithibitika kutenda kosa atatozwa faini ya dola za Marekani 3000.
Aidha, imeelezwa kwamba pamoja na kifungu cha 211 cha sheria hiyo kuwataka wamiliki wa meli na nahodha kuhakikisha idadi ya watu wanakuwemo ndani ya meli kulingana na idadi iliyotajwa ndani ya cheti cha usalama wa meli ya abiria sheria hiyo imekuwa ikipuuzwa na wahusika na watendaji wa serikali Zanzibar.
Hata hivyo hali hiyo imedaiwa inachangiwa na tataizo la uhaba wa ukaguzi jambo ambalo linasababisha uzidishaji wa abiria, hasa kwa meli na boti zinazotoa huduma za usafiri wa ndani wa baharini.
Kuhusu kuzimika boti mbili kuharibika injini zikiwa njiani, Mkurugenzi wa Shirika la bandari Zanzibar (ZPC), Mustafa Aboud Jumbe, alisema wanasubiri ripoti ya ukaguzi ya Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa sheria mamlaka hiyo ndiyo yenye jukumu la kufanya ukaguzi wa boti kesi kama hizo zinapotokea ili kujua chanzo cha boti hizo kuharibika njiani.
Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad amesema uzembe umechangia kuzama kwa meli hiyo kwa sababu ilibeba abiria na mizigo kupita kiwango.
“Meli ilizama kabla ya kuondoka katika bandari ya Malindi abiria walikua wengi na Serikali itachuguza na kuchukua hatua,” alisema Maalim Seif wakati akitoa mkono wa pole kwa wafiwa.
Hata hivyo, Baraza la usalama la taifa limeagiza Mamlaka ya Usafirishaji nchi kavu na ardhini Sumatra na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) wanatekeleza majukumu yao kwa kushirikiana, ili kuepusha majanga kama hayo kwa siku zijazo.
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Muungano, Luhanjo alisema kuwa viwango vya ukaguzi wa vyombo vya usafiri baharini nchini lazima vinafafana katika mamlakla hizo na kuwepo utaratibu wa kubadilishana taarifa ili kuhakikisha usalama unazingatiwa katika sekta hiyo .
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Mimi sipingi uamuzi wa baraza ka wawakilishi, isipokuwa walitakiwa watoe muda wa kutosha kwa SUMATRA ifanye kazi Visiwani hadi hapo ZMA itakapokuwa imejijenga na kupata uwezo wa kutosha. Nimepongeza kauli ya baraza la usalama la taifa kuzitaka mamlaka hizo zishirikiane kwani hiyo ni njia muhimu itakayosaidia ZMA kupata uwezo mzuri. Japokuwa kwa maoni yangu bado naamini kuwa katika masuala ya usalama wa majini na anga serikali ya jamhuri ya muungano ndiyo ipewe dhamana ili kusiwe na sheria mbili zitakazo kinzana. Kwa mfano watumiaji wa vyombo vya majini au usafiri mkubwaa wa abiri na mizigo upo kati ya zanzibar na Dar, sasa hapo tunaona kuwa baraza la wawakilishi halikufanya maamuzi makini kwani ni wazi unapotoka Dar unakuwa unaviwango na mamlaka nyingine kabisa na ile utakayoitumia kutoka Zanzibar. Pili, ZMA imeanzishwa kwa fedha za walipa kodi, ZMA itaendelea kutumia fedha za walipa kodi ambazo zingeweza kuelekezwa katika shughuli au mahali pengine panapohitaji fedha kama vile kuimarisha hspt ya mnazi mmoja ili iweze kuwahudumia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kusafiri kwenda Dar kufuata matibabu. Kazi hizo zingeweza kufanywa na SUMATRA na kushare cost and benefits. Zaidi ya hapo sasa hivi kunasheria (sina uhakika kama wawakilishi wameipitisha au la) kuanzisha Zanzibar Civil Aviation Authority, hii authority au mamlaka ndiyo itasimamia masuala ya usafiri wa anga zanzibar, again naona maamuzi hayo haya faida kwa wananchi wa zanzibar kwa sasa hivi as priorities zao haziko katika usafiri wa anga, ni pesa za wananchi zitatumika kuanzisha ZCAA na labda wawakilishi au jamaa zao watakuwa kwenye bodi au kufanya kazi huko. Na haya mambo yaliyojengeka Znanzibar kila kitu business as usual inaweza kuleta matatizo na huko kwenye mambo ya anga. Bado naamini TCAA ya Muungano ni chombo imara na madhubuti na ndiyo kitakachosimamia ipasavyo shughuli za anga.
ReplyDelete