Na Pili Ali, MCC
WANANCHI wametakiwa kuwatumia wasaidizi wa huduma ya sheria walio katika majimbo ambao wataweza kuwasaidia kuwapa ushauri wa mambo mbali mbali yanayohusu sheria.
Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha huduma za Sheria Zanzibar, Harusi Miraji Mpatani alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Migombani mjini hapa.
Alisema ni vyema wananchi kuwatumia wasaidizi hao wa sheria kwani ni watu walio karibu nao na wataweza kuwapa msaada wa kuwatatulia matatizo yao mbali mbali yanayohusu sheria ikiwemo kupata ushauri.
Aidha alieleza kuwa kituo cha huduma za sheria Zanzibar kinawapatia mafunzo ya sheria za msingi wasaidizi wa huduma hiyo ili waweze kutoa msaada kwa jamii ambao hukabiliwa na matatizo na kushindwa kujua wapi wanaweza kupata msaada.
Kaimu Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa utaratibu wa kuwapeleka wasaidizi wa sheria majimbo ulianzishwa mwaka 2007, katika majimbo yote ya Zanzibar ambapo kila jimbo lina msaidizi wa na sita wapo katika vikosi vya SMZ.
Hata hivyo alisema kwamba lengo la kuanzisha huduma hiyo katika majimbo ni kuwasaidia wananchi kuepuka kufuata masafa marefu ya kufuata huduma za sheria.
Alisema wasaidizi hao wanafanya kazi vizuri kwa wanajamii kama inavyotakiwa kwa kuwaongoza na kuwapatia ushauri wa sheria juu ya masuala mbali mbali.
Kaimu huyo alisema kuwa tangu kuanzishwa huduma hiyo hakuna taarifa yeyote iliyoripotiwa kituoni hapo kutoka kwa wasaidizi hao ambayo inakwenda kinyume na utaratibu wa sheria zilizowekwa.
Kaimu huyo alisema hadi sasa wameweza kuripoti zaidi ya kesi 1,500 za madai ambapo kesi nyingi zinahusiana na migogoro ya ardhi.
Jamani, hebu anaewajua hao wasaidizi wa sheria wa majimbo waliotajwa anisaidie wa majimbo yafuatayo na majina yao;Jang'ombe,mw'kwerekwe na fuoni. Natanguliza shukurani.
ReplyDelete