Habari za Punde

WEZA WAPOTEZA 195 AJALI YA M V SPICE

na Mwandishi wetu

IMEBAINIKA kuwa watu 195 waliopoteza maisha yao katika ajali ya meli ya MV Spice Islander wanatoka katika familia zinazonufaika na Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (WEZA).


Ofisa Mradi wa WEZA Pemba, Zuwena Khamis Omar, amesema kati ya watu hao waliokufa, wanawake ni saba na watoto 188 wanaotoka katika familia 120 za wanawake na wanaume wanaonufaika na WEZA.

Amesema wanamradi hao wa WEZA wamepoteza ndugu zao wa karibu takriban 177 wakiwemo mama, baba, mume, wakwe, kaka, wajomba na shangazi.

Alisema watu 14 kutoka katika familia 12 za wanachama wa mradi huo wameokolewa.

Mradi wa WEZA ulioanza mwaka 2008 umenufaisha watu 7,842 kutoka mikoa ya Kaskazini Pemba na Kusini Unguja kwa kuwajengea uwezo wa kuendesha miradi ya kiuchumi na kukabili matatizo ya kijamii kama kuzuia ukatili wa kijinsia, mambukizi ya virusi Vya ukimwi na mimba mashuleni.

Zuwena alisema wanawake hao wanaotoka katika shehia 28 za mkoa wa Kaskazini Pemba baadhi yao wamepoteza hadi watoto watatu wa kuwazaa.

Alimtaja mmoja wao, Mkitu Ali Hamad, ambaye watoto wake watatu na wengine wanne wa dada yake wamekufa katika ajali hiyo ya meli.

Mkitu ametaka serikali iwachukulie hatua kali wale wote waliofanya uzembe uliosababisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo imeua watu wengi.

“Msiba huu nimeupokea kwa mshtuko mkubwa na kinachotusikitisha zaidi ni kuwa hatukupata kuziona maiti zetu na makaburi yao,” alisema Mkitu.

Zuwena amezitaka taasisi na mashirika ya kijamii yenye utaalam wa ushauri nasaha (huduma shufaa) kutembelea kaya zilizofiwa na watu kwenye ajali hiyo na kutoa huduma hiyo kwa sababu wengi bado wana msongo wa mawazo na uchungu mkubwa.

Mradi wa WEZA pamoja na kuwapa pole wale wote walioathiriwa na ajali hiyo, wameitaka Serikali kudhibiti vyombo vya usafiri wa baharini ili kuepusha maafa makubwa kutokea tena.

Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa mashirikiano kati ya Care Tanzania, Chama cha Wanahabari Wanawake Nchini (TAMWA), Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Austria na Care Austria.

CHANZO: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.