Na Abdi Suleiman, Pemba
MAKOCHA wanaofundisha klabu kubwa za soka hapa Zanzibar, wameshauriwa kujitolea kuwanoa vijana wanaocheza madaraja ya Central, ili kuinua uwezo wa wanasoka hao chipukizi.
Wadau mbalimbali wa soka kisiwani Pemba waliokuwa wakijadili na kutafakari njia bora za kukuza soka la vijana nchini kwenye uwanja wa Gombani, walisema walimu hao wana nafasi kubwa kusaidia kuwajenga vijana kiuwezo ili wafikie daraja za kimataifa.
Ili hilo liweze kufanikiwa, wadau hao walisema iko haja kwa makocha hao kuwa na utaratibu wa kupita viwanjani kwa nia ya kuona mwenendo wa soka la vijana, ili waelewe ni maeneo gani watakayoweza kuwasaidia.
"Wakifanya hivyo, bila shaka wataweza kurekebisha kasoro na kuonesha njia na mbinu za kufuata ili soka la vijana lipate hadhi kulingana na wakati wa sasa, jambo litakalosaidia kupatikana timu za taifa zilizo bora katika umri tafauti", walieleza wadau hao.
Kwa upande mwengine, walifahamisha kuwa, ukosefu wa viwanja vya uhakika, umekuwa ukirudisha nyuma jitihada za kuinua soka hilo, hivyo wakapendekeza kutengwa uwanja maalumu kwa ajili ya vijana wanaochezea madaraja ya Central, Junior na Juvenile.
Hata hivyo, wadau hao wameeleza kusikitishwa na uteuzi wa timu ya kombaini ya Pemba, iliyoshiriki michuano ya Urafiki iliyomalizika hivi karibuni, wakidai vijana wengi waliokuwemo katika kikosi hicho walikuwa na umri mkubwa, jambo lililowanyima fursa wale wanaostahiki.
Walishauri kuwepo utaratibu wa kila wilaya kisiwani humo kuunda timu ya kombaini, na baadae kuanzishwa mashindano yatakayozikutanisha timu za wilaya zote, kutoka madaraja ya Central, Junior na Juvenile hatua waliyosema itasaidia kuinua vipaji vya wachezaji wa umri mdogo.
No comments:
Post a Comment