Habari za Punde

VIWANJA VYA LIGI HAVINA UBORA, USALAMA

Na Donisya Thomas

CHAMA cha soka Zanzibar (ZFA), kimetakiwa kuangalia uwezekano wa kuwa na viwanja bora vya kuchezea ligi ili kuwahakikishia waamuzi na wachezaji usalama wao wakati wote wa mchezo.

Meneja wa klabu ya Malindi Mohammed Masoud aliyekuwa akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema wakati ZFA ikihaha kusaka wafadhili wa ligi, pia wanapaswa kuangalia hali ya viwanja vinavyotumika katika michezo ya ligi hizo.


Alisema viwanja vinavyoendelea kutumika sasa, havina ubora wala usalama kwa waamuzi na wachezaji, hivyo ni vyema ZFA iwe makini kuliangalia jambo hilo kabla ya kupanga ratiba zake.

Masoud alitolea mfano wa ligi hiyo kuchezwa katika viwanja vya Mwanakombo na Fuoni, akidai havina ubora wala usalama kwa wachezaji, waamuzi na hata watazamaji, na kwamba kuruhusu vitumike, kunaonesha ni kiasi gani ZFA haikujipanga na haiko makini katika utendaji wake.

"Mpira wa Zanzibar hauwezi kuendelea kwa kutegemea viwanja kama hivyo, lakini hili linatokana na ukweli kwamba chama kinachosimamia soka hakiko makini", alieleza.

Aidha alifahamisha kuwa viingilio katika viwanja hivyo, nalo ni tatizo kubwa kwani kutokuwa makini kwa ZFA, kunasababisha kupatikana mapato kidogo huku watu wenye fedha na nyadhifa wakiachiwa kuingia bure na wale wasiokuwa na kitu kulazimishwa kulipa kiingilio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.