Habari za Punde

TASWA ZANZIBAR YAMLILIA MAULID

 Uongozi wasema alikuwa kisima cha busara, upendo, ushirikiano

Na Salum Vuai, Maelezo

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar (TASWA-ZANZIBAR), kimesema kuwa, kifo cha Makamu Mwenyekiti wake Maulid Hamad Maulid, kimeacha majonzi makubwa na pengo litakalokawia kuzibwa.

Maulid (54), alifariki jana asubuhi nyumbani kwake Jang'ombe, baada ya kupambana na maradhi ya moyo kwa muda mrefu, ingawa alizidiwa wiki za hivi karibuni na kuwahi kulazwa mara kadhaa katika hospitali za Al-Rahma na Mnazimmoja kwa vipindi tafauti.


Katibu Mkuu wa chama hicho Donisya Thomas, amesema mchango wa marehemu katika kukifanya chama chao kisimame kwa miguu yake, ulikuwa mkubwa na wa manufaa kwa wanachama wote.

Thomas, alimuelezea Makamu Mwenyekiti huyo kuwa ni mmoja wa watu adimu aliyekuwa na upeo na busara za uongozi, kwani alitumia nafasi yake kuwaunganisha wanahabari wachanga ambao walimuona kama baba, kaka na mwalimu kwao.

"Daima alikuwepo kutuongoza na kamwe hakuwa na uchoyo wa kuwapa miongozo waandishi wanaochipukia, na pale alipohisi kuwepo dalili ya mivutano au kutokuelewana kati yao, alikuwa mwepesi kubaini na hakusita kuwarudisha kwenye mstari", alifafanua Thomas huku akionesha huzuni kuu.

Aidha alisema kwamba marehemu Maulid katika uhai wake na tasnia ya uandishi, alikuwa jasiri aliyeamini alichokisimamia, na hakufurahi kuona jitihada zake na za wenziwe katika kusaka mafanikio zinakwama njiani.
Katibu huyo alikumbuka jitihada za marehemu Maulid wakati TASWA-ZANZIBAR, ambaye alizaa wazo la kuwazawadia wanariadha wa timu ya taifa ya Zanzibar waliofanya vyema kwenye mashindano ya kanda ya tano Afrika Mashariki mwezi wa Julai, akisema hafla hiyo ilisaidia sana kukitangaza chama hicho.

"Ni msiba mkubwa na mzito kwetu, na tasnia nzima ya uandishi, na wananchi wa Zanzibar ambao alipenda kuwatetea kwa kufichua matendo maovu yafanywayo na watendaji wasiopenda haki hasa katika migogoro ya ardhi", alisema.

Naye Mratibu wa TASWA-ZANZIBAR kisiwani Pemba Masanja Mabula, amesema waandishi wa habari za michezo Pemba, wamepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa, na kwamba njia pekee ya kumuenzi, ni kuendeleza mema yote aliyokuwa akiyafanya pamoja na wenzake.

"Katika kumuenzi, hatuna budi kuyaendeleza mazuri aliyoyaanzisha ikiwa pamoja na kukiimarisha chama chetu kwa manufaa ya wanamichezo wote wa Zanzibar na Tanzania", alisema Mabula.

Mazishi ya Maulid ambaye alikuwa mwandishi wa kituo cha ITV na Redio One, yanatarajiwa kufanyika leo asubuhi kijijini kwao Bumbwini Misufini Wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.

Uongozi wa chama hicho umetoa mkono wa pole kwa familia yake, wanahabari, wanamichezo na wananchi wote kwa jumla na kutaka wawe na nyoyo za subira, kwani njia aliyoifuata ni ya kila mmoja.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Maulid pahala pema Peponi, Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.