TAASISI ya ‘Busara Promotions’, imeanza kutangaza majina ya wasanii watakaopamba Tamasha la Sauti za Busara’ la mwaka ujao.
Taarifa zilizonaswa kupitia tovuti ya taasisi hiyo, zimewataja baadhi ya wasanii hao na vikundi kutoka ndani na nje ya Zanzibar kuwa ni, Kidumbaki JKU, Shirikisho Sanaa, Skuli ya Kiongoni, Swahili Vibes Band, Tandaa Traditional Group, Tausi Women Taarab, Utamaduni JKU, na Wanafunzi wa SOS (Zanzibar).
Vikundi na wasanii kutoka Tanzania Bara waliothibitisha kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Ally Kiba, Jembe Culture Group, Leo Mkanyia, Lumumba Theatre Group, Seven Survivor na Tunaweza Band.
Aidha kutoka Afrika Kusini ni Tumi & The Volume, Teba Shumba na EJ von Lyrik, ambapo kikundi cha Nneka kinakuja kutoka Nigeria.
Wasanii wengine na nchi watokazo zikiwa kwenye mabano ni Ary Morais (Cape Verde), Chébli Msaïdie (Comoro), Companhia Nacional de Canto e Danҫa (Msumbiji), Hanitra (Madagascar) na Kozman Ti Dalon (Re-Union).
Aidha watakuwepo Ndere Troupe, Qwela kutoka Uganda, Ogoya Nengo (Kenya) pamoja na Super Mazembe (DRC/Kenya).
Busara imethibitisha kuwa miaka minane iliyopita tamasha hilo lilikuwa la kusisimua, ambapo limetajwa kuwa katika daraja la kwanza kati ya matamasha ya muziki ya Afrika chini ya anga la bara hilo.
Tamasha lijalo la Sauti za Busara ambalo ni la tisa, limepangwa kuanza Februari 8 mpaka 12, 2012 katika viwanja vya Ngome Kongwe, ambapo kama kawaida yake, litanogeshwa kwa maandamano makubwa katika mitaa ya mji wa Zanzibar siku ya ufunguzi.
Maandamano hayo yataambatana na ngoma za utamaduni ikiwemo beni, mwanandege na nyenginezo.
Kivutio chengine ni filamu za muziki wa Afrika, soko katika tamasha, na kwa siku nne hizo kutafanyika pia semina za mafunzo, Busara Xtra na kadhalika.
No comments:
Post a Comment