BAADA ya kilio cha muda mrefu kuomba udhamini wa ligi za soka za vijana, hatimaye Kamati ya Central Taifa imepata ahueni kutoka kwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Umoja huo UVCCM, umeikabidhi kamati hiyo shilingi milioni moja kugharamia zawadi za washindi, wachezaji bora na waamuzi wanaochezesha ligi ngazi ya Junior Taifa inayoendelea sasa.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana kwenye ofisi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) zilizoko hoteli ya Bwawani, ambapo Naibu Katibu wa UVCCM Taifa, Zanzibar Jamal Kassim alitanguliza shilingi laki tano kwa Katibu wa Central Taifa Abdallah Thabit.
Kabla kukabidhi fedha hizo, Kassim alisema umefika wakati sasa kwa mamlaka za soka nchini, wafadhili, kampuni na wadau wengine, waone umuhimu wa kuwekeza katika soka la vijana ili kujenga msingi imara wa kuwa na timu za taifa.
Alisena njia hiyo pekee, ndiyo itakayoifanya Tanzania iondokane na aibu ya kuitwa kichwa cha mwendawazimu, kwani nchi imejaaliwa hazina kubwa ya vipaji vinavyohitaji kuendelezwa kwa kupewa misaada mbalimbali na kuwekewa mazingira mazuri.
“Kwa miaka mingi sasa jitihada za nchi yetu kujikwamua na aibu ya kufanya vibaya katika ngazi ya kimataifa zimegonga ukuta kwa kuwa hatujaona haja ya kuvitumia vipaji vya wachezaji chipukizi, tubadilike”, alifafanua Naibu Katibu huyo wa UVCCM.
Akitoa shukurani zake kutokana na msaada huo, Katibu wa Kamati ya Central Taifa Abdullah Thabit, alieleza matarajio yake kuwa msaada huo utawashajiisha wadau wengine kuzitupia jicho ligi za watoto ambazo ndizo zinazozalisha wachezaji wa kuzichezea klabu kubwa na timu za taifa.
No comments:
Post a Comment