Habari za Punde

DK SHEIN AFANYA MAZUNGUMZO NA KIONGOZI WA RAS AL KHAIMAH SHEIKH SAUD BIN SAQR ALQASIMI

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na mwenyeji wake kiongozi wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi na kufanya mazungumzo yaliolenga kukuza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.

Mazungumzo hayo yaliofanyika katika Kasri ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi ililopo mjini Ras-Al-Khaimah, viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya kukuza uhusiano na kuimarisha mashirikiano katika kuinua seka za maendeleo ikiwemo uwekezaji, biashara, viwanda, elimu, Maeneo huru ya Uchumi, Afya na Uwezeshaji wananchi kiuchumi.


Aidha, viongozi hao walizungumza juu ya sekta za maendeleona katika kuimarisha mashirikiano kwenye sekta nzima ya maeneo huru na uwekezaji sanjari na bandari huru.

Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na mwaliko wake na kusisitiza kupongeza mafanikio yaliopatikana nchini humo kwa kipindi kifupi.

Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras-Al-Khaimah.

Nae Kiongozi huyo alieleza kuwa Ras-AlKhaimah itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Ras-el-Khaimah zina historia kubwa katika nyanja ya kibiashara hivyo hatua zaidi zitaimarishwa kwa pamoja katika kukuza sekta hiyo pamoja na sekta ya uwekezaji.

Wakati huo huo Zanzibar na Ras-Al-Khaimah imesaini Mkataba wa Makubaliano juu ya Ushirkiano katika sekta mbali mbali za maendeleo, saini hiyo ilishhudiwa na Rais Dk. Shein pamoja na Sheikh Saud Bin Al Qasimi huko katika ukumbi wa Kasri ya Sheikh Saud.

Kwa upande wa Zazibar Waziri wa Kazi, Uwezeshaji , Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mhe. Haroun Ali Suleiman alisaini ambapo kwa upande wa Ras-Al-Khaimah aliyetia saini ni Sheikh Abdalla Bin Humaid Al Qasimi.

Miongoni mwa makubaliano hayo ni pamoja na kuendeleza Maeneo Huru ya Uchumi, Bandari Huru ambapo itaifanya Zanzibar kuwa Kituo Kikuu cha Biashara, ushirikiano wa kitaalamu, kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu katika nyanja za afya, nishati, huduma za afya, ufundi.

Aidha, utafiti juu ya vianzio vya maji, mashirikiano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwawezesha wananchi Kiuchumi na kuendeleza ajira pamoja na mambo mengineyo

Pia, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara wa Ras-Al-Khaimah na kueleza kuwa muendelezo wa biashara kati ya Zanzibar na Ras-Al-Khaimah ndio msingi kubwa ya uhusiano uliopo.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kupata maelezo kutoka kwa Jumuiya ya Wafanyabishara wa Ras-Al-Khaimah

Alieleza kuwa ziara hiyo imelenga katika kukuza uhusiano wa kibiashara, viwanda, uwekezaji kati ya Ras-Al-Khaiman na Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vivutio vingi vya Utalii ambapo juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuiimarisha sekta hiyo.

Dk. Shein alieleza kuwa ziara hiyo ni ya kidugu na inaimarisha zaidi historia ndefu baina ya Zanzibar na watu wa Ras-Al-Khaiman.

Wakitoa maelezo yao wafanyabishara hao walieleza kuwa Ras-Al-Khaimah ina mambo mengi ya kushirikiana na Zanzibar na kusisitiza kuwa iko tayari kuendeleza uhusiano na udugu wao kwa kuimarisha sekta za maendeleo.

Walieleza kuwa miongoni mwa sekta ambazo wako tayari kushirikiana ni pamoja na sekta za uwekezaji, viwanda, biashara na nyenginezo na kusisitiza kuwa Zanzibar imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya Utalii, hivyo nao wana mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar.

Dk. Shein akiwa na ujumbe wake pia, alitembelea Chuo Kikuu cha Sayansi cha Ras-Al-Khaiman, Hospitali ya rufaa ya Ras-Al-Khaiman pamoja na kutembelea kiwanda cha dawa cha JULPHAR, alitembelea Maeneo Huru ya uwekezaji RAKIA ambako huzalisha bidhaa mbali mbali zikiwemo tiles, vyombo vya nyumbani na vyenginevyo.

2 comments:

  1. Waswahili husema nia njema hairogwi, inaamanisha hizi ahadi tuu ambazo Zanzibar imezipata tangu utawala wa Dr Shein kuanza basi kama zinatekelezwa basi inatosha kuifanya Zanzibar kujiweza kuichumi. Nafikiria ni busara pale ambapo ahadi hizi hazitekelezwi Serikali ikachukukua hatua za makusudi ku-review policy yake na kuona hasa ni vitu gani vimekuwa ni kikwazo. Kuliko kufanya ziara nyengine, kwa mfano katika nchi ambayo hata umeme na maji ya uhakika haina. huenda ikawa ni moja kati ya vipingamizi vya maendeleo hasa katika sekta ya uekezaji wa viwanda ni bora tukawa realistic.

    ReplyDelete
  2. Naungana na mchangiaji mia kwa mia kwamba tumekuwa nchi ambayo hatuna mwelekeo katika suala la maendeleo na vipi wenzetu walifika walipofika.

    Ziara ya nchi ya Mauritius ilikuwa somo zuri kwetu kwani kile ni kisiwa kama sisi na Utalii ni kitengo kimoja muhimu kwa nchi ya Mauritius.

    Nchi kama Seychelles, Madagscar hata Visiwa vya Comoro ni Sehemu za kuzingatia katika kujifunza vipi wenzetu wameweza kuwa na maendeleo angalau ya kuweka infrastructure tu kwani vyengine haviji bila ya kuwekewa misingi. Na hiyo misingi ndiyo hatunayo (Umeme wa uhakika, maji safi na Salama, Mawasiliano na kadhalika)

    Shukran mchangiaji kwa hoja ya haja

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.