Habari za Punde

'KATIBA MPYA FURSA ADHIMU ZANZIBAR KUAMUA' MAALIM SEIF

KATIBU Mkuu wa CUF, ambae ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wananchi wa Donge Mchangani, alipofanya ziara ya kutembelea majimbo ya Kitope, Bumbwini na Donge wilaya ya Kaskazini B, Unguja jana. (Picha na Salmin Said, OMKR)


Hassan Hamad, OMKR

KATIBU Mkuu wa Chama Cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wazanzibari waungane na kuwa na kauli moja wakati wa kutoa maoni juu ya katiba mpya ili kupata mfumo wa muungano wanaoutaka.

Maalim Seif amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara huko Donge mchangani Wilaya ya Kaskazini B Unguja jana.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein atateuwa wajumbe wa tume ya kuchukua maoni ya wananchi juu ya katika mpya wanayoitaka ambapo wananchi wa Zanzibar pamoja Tanzania bara watapata fursa sawa za kueleza maoni yao.



Alisema kwamba katika hatua hiyo iwapo wazanzibari watakuwa na kauli moja juu ya mambo wanayotaka yawemo au yasiwemo kwenye katiba hiyo, Tanzania bara hawatokuwa na njia nyengine isipokuwa kukubaliana na maoni ya wazanzibari, lakini iwapo watatofautitana na kukosa msimamo inaweza kuwaathiri wazanzibari kupata kile wanachokihitaji.

“Hii ni fursa adhimu kwa wazanzibari kupata mambo wanayoyataka ndani ya Jamhuri ya Muungano ikiwemo mfumo wa Muungano wenye maslahi kwa Zanzibar”, alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye pia ametembelea majimbo ya Kitope na Bumbwini, amesisitiza kuwa hiyo ni fursa pekee ya wazanzibari kuamua hatma ya nchi yao ikiwa ni pamoja na kuamua muundo wa muungano wanaoutaka wenye maslahi na Zanzibar na vizazi vijavyo.

Kwa upande mwengine Maalim Seif amewataka wananchi kuendelea kuhifadhi mazingira ili kuvirithisha vizazi vijavyo nchi yenye misitu na neema.

Amesema iwapo juhudi za makusudi hazitochukuliwa kuna hatari kwa vizazi vijavyo kurithishwa nchi ikiwa jangwa, hali ambayo itazorotesha shughuli zao za maendeleo.

Amewataka wananchi wa maeneo hayo kuacha kabisa tabia ya ukataji miti ovyo na kuongeza juhudi katika upandaji wa miti mbali mbali ikiwemo ya matunda, ili kuimarisha rasilimali ya misitu ambayo ni hazina muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Amesema kuwepo kwa miti mingi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakiviathiri visiwa vya Zanzibar kwa kukosa mvua kwa wakati, kuathiri vianzio vya maji na kupoteza rutba na haiba ya visiwa vya Zanzibar.

Akizungumzia dawa za kulevya, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar amewataka wanavijiji kuvihifadhi vijiji vyao na tatizo hilo, kwa vile athari zake zinakuwa kubwa hasa kwa vijana na kupelekea kupoteza nguvu kazi ya taifa.

“Wenyewe wanavijiji tukiamua kudhibiti dawa za kulevya haziingii. Kweli, uongo”, alihoji Maalim Seif.

Kuhusu maendeleo ya wananchi, Maalim Seif amesema Serikali inaendelea na juhudi mbali mbali kuona kuwa tatizo la umaskini linapungua kwa wananchi.

Ametaja baadhi ya juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya saba kuwa ni pamoja na kuyaalika makampuni ya kigeni yakiwemo ya uvuvi kuja kuwekeza Zanzibar, jambo ambalo litapunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Akizungumzia kuhusu vitambulisho vya uzanzibar mkaazi, Maalim Seif amesema suala hilo ni la lazima kwa kila mzanzibari aliyetimia umri wa miaka 18 na awajibika kuwa nacho kwa mujibu wa sheria, vyenginevyo anaweza kuwajibishwa kwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja.

Kwa upande wake mkurugenzi wa haki za binadamu, habari, uenezi, mawasiliano na umma wa CUF, Salim Bimani, amewasisitiza wananchi wa maeneo hayo kufuatilia vitambulisho vya uzanzibari ukaazi, ili kuhakikisha kuwa wanavipata na kuvitumia kwa shughuli mbali mbali za siasa na kimaendeleo.

Kwa mujibu wa Bimani, wananchi wengi hasa wa jimbo la Bumbwini hawajachukua vitambulisho vyao vya uzanzibari mkaazi, licha ya vitambulisho hivyo kuweko katika mamlaka zinazohusika na vitambulisho hivyo.

1 comment:

  1. Duu!...hii picha ya Maalim hapa inathibitisha wazi kua sasa 'kwishne' La msingi, asome alama za nyakati, apunguze ukaidi, aandae mrithi kabla mapinduzi ya ndani ya chama hayajamkumba.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.