Habari za Punde

KUZUIWA SEAGULL HAKUTUSUMBUI - ZFA

Na Mwajuma Juma

LICHA ya kuzuiwa kwa meli ya Seagull kufanya safari zake, Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kimesema kuwa kimejipanga vyema kuhakikisha hakikwami kuzisafirisha timu zinazoshiriki ligi kuu kati ya Pemba na Unguja.

Seagull imezuiliwa kutoa huduma za usafiri kati ya visiwa vya Zanzibar na Tanzania Bara, baada ya kubainika haiku katika hali ya kuridhisha kufuatia malalamiko ya baadhi ya wasafiri.


Msemaji wa chama hicho Hafidh Ali Tahir, amewaambia waandishi wa habari kuwa, ZFA iko makini na ligi kuu itakapoanza Jumatano ijayo, kutakuwa na usafiri wa uhakika kuzibeba timu shiriki.

“Hatujatetereka, suala la usafiri si tatizo kwetu kwani tayari tumeshatafuta usafiri mwengine utakaowahudumia wachezaji wa timu zinazoshiriki ligi hiyo”, alisema Tahir.

Sambamba na hilo, alisema ZFA inakusudia kufanya mabadiliko kwa upande wa waamuzi, kwa kuwachanganya wa Unguja na Pemba katika kituo kimoja ili kuondosha malalamiko yasiyo ya lazima.

Baada ya kumalizika kwa kadhia ya timu ya Malindi, ratiba ya ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya usafiri wa baharini Seagull, itatolewa wiki ijayo, ingawa imeshaeleweka kuwa katika uwanja wa Mao Dzedong, timu zitakazotoana jasho Novemba 23, ni Miembeni asili na Miembeni United.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.