Habari za Punde

MAALIM SEIF AIKABIDHI LESENI STAR TIMES AITAKA KUANDAA VIPINDI VIZURI

Na Faki Mjaka –Habari Maelezo Zanzibar 24/11/2011

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameutaka uongozi wa Kampuni ya Kichina ya Star Times kuandaa Vipindi vizuri katika Channel zao ambavyo vitakuwa havina athari mbaya kwa silka na tamaduni za Zanzibar.

Ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa hotuba yake katika sherehe ya kuikabidhi Leseni Kampuni hiyo itakayoiwezesha kufanya kazi zake Zanzibar katika sherehe iliyofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort.


Leseni hiyo iliyotolewa na Tume ya Utangazaji Zanzibar kupitia kwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Joseph Kilangi kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo itakuwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa kuanzia.

Maalim Seif amesema Zanzibar ni nchi ambayo ina Silka na tamaduni zake ambazo zinafaa kulindwa hivyo hatarajii uanzishwaji wa Kampuni hiyo Zanzibar kuwa utakuwa kichocheo cha kuharibu utamaduni wake.

Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itashirikiana bega kwa bega na Kampuni hiyo ili kuiwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi ya kutoa huduma hasa katika nyanja za habari.

Aidha amesema kuanzishwa kwa Kampuni ya Star Times Zanzibar kutawawezesha Wazanzibari wengi kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa Teknolojia hasa katika Nyanja za habari jambo ambalo litawapelekea kupata taarifa mbalimbali kwa wakati.

Amesema mahitaji ya kupata habari yanaongezeka siku hadi siku duniani na kwamba Star times inaweza kuwa kichocheo cha kukuza demokrasia Zanzibar na ukuwaji wa haki ya kupata taarifa.

Maalim Seif amesema China kama ilivyokuwa nchi nyengine inakaribishwa kuendelea kuwekeza Zanzibar katika sekta mbalimbali hasa kutokana na usalama uliopo na ushirikianao wa Serikali kwa Wawekezaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Star Times Pang Xin Xing ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwapatia Leseni ya kufanya kazi Visiwani Zanzibar ambapo watatoa huduma hiyo kama ilivyokuwa katika Nchi nyingine.

Amesema Kampuni ya Star Times inatarajia kuanza kazi kabla ya June mwakani na kwamba tayari wamesambaza huduma zao katika mikoa saba ya Tanzania Bara miongoni mwao ni Dar es Salaam, Tanga, Dodoma Arusha na Mbeya.

Mapema akitoa Maelezo mafupi Mkurugenzi wa Utumishi wa Wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Joseph Kilangi kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar amewaomba wawekezaji wengine kuja Zanzibar kuwekeza na kuitaka Star Times kupunguza gharama kwa Vifaa ambavyo wananchi watawajibika kununua.

Mapema ujumbe huo wa watu 13 uliowasili Zanzibar leo asubuhi na kuongozwa na Naibu wa Waziri wa Mamlaka ya Redio,Televisheni na Filamu Li Wei ulitembelea Chuo cha Habari Zanzibar na kuona jinsi chuo hicho kinavyofundisha lugha ya Kichina ambapo pia Naibu Rais wa Radio China Kimataifa Wan Yunpeng na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Han Mei walikuwepo.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.