Na Haji Nassor Pemba
WACHEZAJI wa mpira wa wavu wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba , wametupa shutuma nzito kwa viongozi mbalimbali wa michezo, kutokana na kutoushughulikia ipasavyo mchezo huo na kuanza kupoteza muelekeo wilayani humo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wachezaji hao walisema wamekuwa hawajui lipi la kufanya ingawa wameamua kujikusanya na kuendeleza mchezo huo kwa zaidi ya miaka 25 sasa bila ya mafanikio yoyote.
Walisema timu yao ipo takribani robo karne sasa, lakini hawajapata msaada wowote kutoka wa viongozi wa michezo wakiwemo wabunge, wawakilishi, lakini wamekuwa wakitoa majibu yasio sahihi na ahadi zisizotekelezeka.
Mmoja kati wachezaji hao Juma Faki, alisema kwa muda mrefu sasa wanakabiliwa na tatizo la uwanja, jezi, mipira na hata kukosa mkufunzi wa kudumu juu ya mchezo na kusababisha kuanza kupoteza vijana pole pole.
Alieleza, kwa sasa wamekuwa wakinolewa na kijana mmoja ambae si wa uhakika na kuwapa mafunzo wiki mara moja, kwa vile ni mfanyakazi Serikalini, hivyo hutegemeana na muda anaorudi kazini.
“Uwanja tulionao ni watope na wakati mwengine hujaa maji na kushindwa kuchezeka, lakini hilo si tatizo, lakini kubwa ni kukosa mtaalamu wa kutufunza na kupeleka kucheza bila ya kufahamu sheria”, alieleza Juma.
Nae Suleiman Ameir, alisema, kwa sasa wamekuwa wakifanya mazoezi kwa njia ya kujishibua kutokana na wanaofahamu sheria na kanuni za mchezo huo kuvunjika moyo baada ya viongozi husika kuutelekeza mchezo huo.
Afisa Michezo wilaya ya Mkoani, Mohamed Juma, hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia kadhia.
Timu hiyo ya mpira wa wavu ya Mkoani hivi karibuni ilishiriki michuano ya mchezo huo Zanzibar na kushika nafasi ya mwisho jambo ambalo lilichangiwa na kukosekana kwa mwalimu na ari ya vijana wenyewe.
No comments:
Post a Comment