RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua juhudi za kila aina katika kuhakikisha karafuu za Zanzibar zinaongezeka thamani na kuendelea kutambuliwa Kimataifa.
Dk. Shein alieleza hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulikia hati miliki WIPO, pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Biashara ITC, zote zenye makao makuu yao Geneva nchini Switzerland.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza kuwa karafuu za Zanzibar zina historia kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki hadi dunia nzima na kusisitiza kuwa kutokana na hali hiyo serikali imeamua kwa makusudi kuendelea kulipa hadhi ya kipekee zao hilo.
Alieleza kuwa kuliimarisha zao la karafuu na kuweza kutambulika kimataifa sanjari na kuliongezea thamani kutalipelekea zao hilo kuendelea kuchangia uchumi wa Zanzibar.
Alisema kuwa serikali imeamua kuchukua hatua za makusudi za kulipandisha bei zao la karafuu kwa wakulima hatua ambayo imeleta faraja kubwa kwao na kueleza kuwa juhudi za kulifanya kuwa na hadhi ya kipekee ‘branding’ kutasaidia pia, kuongezeka kwa bei ya zao hilo katika soko la dunia.
Aidha, Dk Shein alipongeza juhudi za pamoja zilizochukuliwa na wataalamu hao pamoja na Wizara husika ambazo mchakato wake umeanza tokea mwaka 2009, na kueleza kuwa serikali imekusudia kuleta mabadiliko makubwa kwa karafuu za Zanzibar.
Mapema Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Mazrui alimueleza Rais Dk. Shein kuwa kumekuwa na mashirikiano mazuri kati ya Wizara na Taasisi hizo za Kimataifa na kueleza kuwa ujumbe huo upo Zanzibar kwa muda wa siku mbili ukiendelea na mchakato wa kuipa hadhi karafuu ya Zanzibar.
Mtendaji Mkuu wa Programu kutoka Shirika la WIPO Neema Nyerere alimueleza Rais Dk. Shein kuwa ujio wao pamoja na mambo mengineyo lengo kubwa ni kuendeleza mchakato wa kuhakikisha karafuu inayozalishwa Zanzibar inakuwa na thamani na hadhi kubwa kimataifa.
Alieleza kuwa kutokana na juhudi hizo za pamoja anamatumaini makubwa ya mafanikio juu ya azma hiyo ambapo kwa upande wa WIPO imeivalia njuga kuhakikisha mafanikio yanapatikana.
Mtendaji Mkuu huyo alieleza kuwa uwezekano mkubwa upo kwa karafuu za Zanzibar kupata hadhi ya kipekee kwani Jumuiya yake ina uzoefu mkubwa kutokana na mafanikio yaliopatika nchini Ethiopia kutokana na zao lake la kahawa ambalo ililivalia njuga na hivi sasa limeweza kuwa na hadhi ya kimataifa.
Nae Bwana Jacky Charbonneau, kutoka Kituo Cha Kimataifa Cha Kibiashara ITC, alieleza kuwa juhudi za pamoja hadi hivi sasa zimeweza kuleta mwanga mkubwa wa matumaini juu ya zao la karafuu za Zanzibar na kusisitiza kwa wakulima kulifanyia mambo ya msingi zao hilo kabla ya kulifanyia ‘branding’.
Alisema kuwa ICT ina matumaini makubwa kuwa karafuu za Zanzibar zitakuwa na hadhi na thamani kubwa kimataifa na kuweza kujitangaza na kupata soko duniani sanjari na kukabiliana na ushindani wa kibiashara.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaki Okada ambao kwa pamoja viongozi hao walisisitiza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili hizo.
Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa Japan kutokana na juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo kuimarisha miundombinu ya umeme, maji na sekta nyenginezo.
Nae Balozi huyo wa Japan aliahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta hizo za maendeleo.
No comments:
Post a Comment