Habari za Punde

TAASISI, MASHIRIKA YAFUATE SHERIA YA MANUNUZI

Na Fatuma Kitima, Dar es Salaam

TAASISI za Umma na Mamlaka zimetakiwa kufuata sheria ya ununuzi wa Umma ili kuweka taratibu, misingi na miongozo ambayo ikifuatwa kikamilifu serikali itapata huduma kama vifaa na miundombinu mbalimbali kulingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Dk. Ramadhan Mlinga alisema kuwa wanunuzi hawataki kufuata sheria zilizopangwa hivyo kusababisha matatizo.


Dk.Mlinga alisema ukaguzi wa shughuli za ununuzi katika Taasisi za Umma unafanywa na PPRA ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali na kuhakikisha sheria ya ununuzi wa umma na kanuni zake unafuatwa na Taasisi za umma zifanyapo manunuzi.

Alisema kuwa kaguzi hizo zinasaidia kujua eneo gani lina matatizo makubwa hivyo kuwawezesha kuweka mikakati ya kufanya maboresho ikiwemo kujenga uwezo wa watumishi wa umma wanaofanya kazi za ununuzi au mapendekezo kwa mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria ikiwa wamekiuka matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma.

Aidha alisema katika kaguzi hizo taasisi zilizokaguliwa ambazo zinafuata sheria ya ununuzi wa umma na kanuni zake ni asilimia 68% ambapo ni wizara , Idara na Wakala zimefanya vizuri zaidi kwa kiwango cha 70% zikifuatiwa na mamlaka za serikali za Mitaa zina kiwango cha 67% ikifuatiwa na Mamlaka ambazo zina kiwango cha 66%.

Hata hivyo alisema kuwa ukaguzi huo umefanyika kwenye taasisi 106 ikiwa Wizara 36 ,Idara na Wakala 51,Mamlaka na Taasisi za Umma,taasisi 19 zikiwa Mamlaka za Serikaliza Mtaa.

Alisema kati ya Taasisi hizo zilizokaguliwa 13 zilifanya vizuri kwa kiwango cha 80% ikiwa taasisi 75 zilikuwa na kiwango cha 50%na 80% ikifuatiwa na taasisi 18 zilizofanya vibaya kwa kiwango cha 50% .

Aidha alisema kuwa miradi iliyotekelezwa vizuri inathamani ya shilingi bilioni 170.2 ikiwa miradi ambayo haikutekelezwa ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 13.8.

Alisema ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2013 hadi 2014 lengo la PPRA ni utekelezaji wa sheria ya ununuzi wa umma unafikia 80% hivyo taasisi zote zinatakiwa kuhakikisha kuwa maeneo ambayo utekelezaji wake ni chini ya 80% yanafanyiwa kazi ili kuboresha utendaji katika maeneo hayo.

Alitoa wito kwa Wakuu wa Taasisi zilizokaguliwa na hata wasio kaguliwa washirikiane na PPRA kuboresha manunuzi yanayofanywa ndani ya taasisi zao na kuhakikisha thamani ya fedha zinazotumiwa kufanya manunuzi zinalingana na ubora wa huduma na vifaa vinavyonunuliwa.

Naye Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema kuwa bado kuna changamoto katika taasisi za umma kutozingatia sheria katika ununuzi wa umma.

Alisema matatizo yanatokea kwa kuwa wanunuzi hawakusoma sheria vizuri na kama wangesoma matatizo yasingekuwepo katika utekezaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.