ZAIDI ya shilingi bilioni 1.6 sawa na asilimia 76.72 zimekusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), tawi la Pemba kwa mwaka wa makusanyo 2010/2011, kati ya shilingi bilioni 2.1 zilizopangwa kukusanywa na Mamlaka hiyo.
Akizungumza mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake, Chake Chake juu ya matayarisho ya maadhimisho ya siku ya mlipa kodi, Mdhamni wa TRA Pemba, Habib Saleh Sultan, alisema kiwango hicho walichokusanya kilitokana na vyanzo mbali mbali.
Alisema kua TRA kwa upande wa Pemba imekua ikijitahidi katika kukusanya mapato kwa mujibu wa vyanzo na maeneo wanayopaswa ambapo fedha zote huingizwa kwenye mfuko wa mkuu wa hazina wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza makusanya hayo sio kidogo hasa kwa vile bado baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa sugu wa kulipa kodi zao kwa hiari na wakati mwengine kusababisha mabishano makali baina yao na wafanyabiashara.
Mdhamini huyo wa TRA Pemba, alieleza kuwa katika mwaka 2009/2010 TRA ilitakiwa kukusanya shilingi bilioni 1.54 na kwa mwaka huo ilifanikiwa kwani wafanyabiashara na walipa kodi wengine walijitutumua na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.3 sawa na asilimia 84.34.
Aidha alieleza kuwa kwenye mwaka wa 2006/2007 TRA ilifanikiwa kuvuka lengo la makusanyo kwani walitakiwa kukusanya shilingi milioni 658.30 ambapo walikusanya zaidi ya shilingi milion 821, ambapo kima hicho ni kikubwa ikilinganishwa na hali za wafanyabiashara walioko Pemba.
Katika hatua nyengine mdhamini huyo alieleza ndani ya TRA kuna idara ya Forodha ambayo kazi yake ni kukusanya mapato yatokanayo na uingizwaji wa biashara za kimataifa "International trade’’ jambo ambalo kwa kisiwani Pemba limekuwa ni zito.
Aliongeza Idara hiyo imekuwa ikishindwa kukusanya ushuru ipasavyo kwa vile wafanyabiashara wanaotoka na mizigo yao kutoka nje ya nchi huishia Unguja na Tanzania bara kwa vile bandari ya Mkoani kutokuwepo kwa huduma timilifu.
"Kama bandari ya Mkoani itaimarishwa na lengo la serikali kufanikiwa la kuimarisha bandari yetu basi hata sisi TRA ukusanyaji wa mapato utaongezeka maradufu, maana tunacho kitengo cha Idara ya Forodha ambacho kazi zake ni miongoni mwa kukusanya kodi za biashara za kimataifa’’,alifafanua Mdhamini huyo.
Hata hivyo alisema kuwa Mamlaka hiyo itaendelea na kutoa elimu kwa walipa kodi ili kila mmoja afahamu umuhimu wa ulipaji na kufikia mahala walipe kodi kwa hiari.
Kwa upande wake Ofisa Forodha kutoka TRA Kisiwani Pemba, Abdallah Hassan Ali aliishauri serikali kuharakisha uimarishaji wa bandari ya Mkoani, ili meli za kigeni na wafanyabiashara waweze kupakua bidhaa zao hapo kwa lengo la kuinua uchumi wa wazanzibari.
"Wakati wowote serikali ikiimarisha bandari ya Mkoani kwa kuwepo huduma muhimu ikiwa ni pamoja na mashine za kupakulia mizigo na hata sehemu za karibu za kuhifadhia mizigo, basi hata mapato yataongeza maradufu’’,alisema Ofisa huyo.
TRA imeanzishwa rasmi mwaka 1995 na kuanza kazi zake mwaka mmoja baadae chini ya sheria namba 11 ya mwaka 1995, ikiwa na majukumu sita ikiwa ni pamoja na kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato yote ya serikali kuu, kuinua kiwango cha uwajibikaji wa hiari wa kulipa kodi.
No comments:
Post a Comment