Habari za Punde

WANAFUNZI 46,489 ZANZIBAR KUFANYA MITIHANI YA TAIFA

Ni kidato cha pili, darasa la saba

Na Husna Mohammed

WANAFUNZI 46,489 wanatarajiwa kufanya mitihani ya darasa la saba na kidato cha pili Unguja na Pemba kuanzia Jumatatu ijayo.

Kati ya wanafunzi hao 25,400 ni wa darasa la saba ambapo watahiniwa wa kidato cha pili ni 21,465.

Kwa upande wa darasa la saba mitihani hiyo itaanza Novemba 16 na 17 mwezi huu na kidato cha pili itakuwa Novemba 21 hadi 26 mwezi huu Unguja na Pemba.


Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari, huko ofisini kwake Mazizini Unguja, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Zahra Ali Hamad, alisema maandalizi kwa ajili ya mitihani hiyo imeshakamilika na kwamba kinachosubiriwa ni siku iliyopangwa tu.

“Maandalizi yote juu ya ufanyaji wa mitihani hiyo yakiwa uchapishaji wa mitihani, usambazaji, uchaguzi wa wasimamizi na usafiri wa wasimamizi yameshakamilika”, alisema.

Naibu Waziri huyo, alitoa wito kwa watahiniwa kutotumia udanganyifu wa aina yoyote katika mitihani hiyo na kwamba atakaebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa mitihani yake.

Zahra alisema pamoja na mambo mengine lakini aliwataka watahiniwa hao kutochukua vifaa vyovyote visivyohitajika katika mitihani ikiwemo simu za mkononi, kutowasiliana na mtu yoyote ndani au nje chumba cha mtihani isipokuwa msimamizi tu.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo aliwataka walimu wote watakaosimamia mitihani hiyo, kutekeleza wajibu wao wa usimamizi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

“Tunaviomba vyombo vya ulinzi vitakavyoshiriki katika ulinzi wa mitihani kuwa macho na watu watakaojaribu kujipenyeza katika maeneo ya skuli kwa nia ya kuwasaidia wtahiniwa kufanya udanganyifu”, alisema.

Aliwataka walezi, wazazi kuwahimiza watoto wao kufika mapema katika vituo vya kufanyia mitihani na kuchukua vifaa vyote vinavyohitajika kama penseli, kalamu, mstari, raba, boksi la kampasi na gamba la kuwekea karatasi ya mtihani ambalo halina michoro ya aina yoyote.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri huyo, aliwataka watahiniwa hao kufuata maelekezo ya msimamizi na wasaidizi wasimamizi wa kituo cha mitihani, pamoja na kuandika nambari sahihi ya mtihani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.