Na Husna Mohammed
MASHINDANO ya judo kuwania ubingwa wa taifa ambayo yanaandaliwa na chama cha mchezo huo Zanzibar (ZJA), yanatarajiwa kufanyika kisiwani hapa Disemba 18, mwaka huu.
Mashindano hayo yatakayoshirikisha wachezaji kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, yamepangwa kufanyika katika ukumbi wa Budokan ulioko Amaan mjini hapa.
Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu Mkuu wa chama hicho ambae pia ni Kocha Mkuu wa mchezo huo Zanzibar, Tsuyoshi Shimaoka, alisema mashindano hayo yanalenga kupata mabingwa wa uzito tofauti na wa jumla, sambamba na kuchagua wachezaji wa timu ya taifa.
Timu ya taifa inayochaguliwa kutokana na mashindano hayo, hushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.
Shimaoka ambaye ni raia wa Japan anayefundisha judo hapa Zanzibar kwa zaidi ya muongo mmoja, alisema pia mashindano hayo yatawashirikisha wachezaji wa kike pamoja na watoto wadogo, kwa nia ya kuibua vipaji vya umri huo.
Alifahamisha kuwa, katika mashindano hayo zawadi kadhaa zitatolewa kwa washindi zikiwemo vikombe na vitu tafauti.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na Konsula Oweno mjumbe kutoka Japan, atakayekuwa mgeni rasmi.
No comments:
Post a Comment