Habari za Punde

ZOEZI LA CHANJO YA WANYAMA LAFANYIKA NDIJANI

Na Husna Mohammed

ZAIDI ya wanyama 300 wa aina mbalimbali wanatarajiwa kuchanjwa leo katika kijiji cha Ndijani, wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Zoezi hilo la kuchanja wanyama ni maadhimisho ya siku ya wanyama duniani inayofanyika Oktoba 4 kila mwaka, ambapo kwa Zanzibar mwaka huu itafanyika leo kutokana na sababu mbalimbali.


Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Jumuiya ya kuzuia ukatili kwa wanyama na utunzaji wa mazingira (ZSPCA), huko Mbuyu mnene Unguja, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Makame Haji Mlenge, aliwataja wanyama hao kuwa ni ng’ombe, mbuzi, mbwa, paka, punda, bata, sungura nakadhalika.

Mwenyekiti huyo alisema zoezi hilo litafanyika katika kijiji hicho na vitongoji jirani kutokana na eneo hilo kuwa na wanyama wengi sambamba na kuteuliwa na Idara ya Uendelezaji wa Mifugo Zanzibar.

“Nadhani wenzetu tunaoshirikiana nao wa Idara inayohusika wamelipa umuhimu mkubwa kutokana na zoezi kama hilo mwaka jana kufanyika Mkoa wa Kaskazini hivyo mara hii litafanyika huko na pia kwa kuwa kuna wanyama wengi ukilinganisha na sehemu nyengine”, alisema.

Aidha Mlenge ametoa wito kwa wananchi wenye wanyama kuwapeleka wanyama wao katika kijiji cha Ndijani Skuli kwa ajili ya kupata chanjo pamoja na kupatiwa matibabu mbalimbali yanayowasumbua wanyama.

Akizungumzia kuhusu historia ya ukatili dhidi ya wanyama, Mwenyekiti huyo alisema wanaekolojia waliweza kutafuta njia ya kuweza kutambua hali mbaya ikliyopo kwa aina za wanyama ambazo zipo hatarini kutoweka.

Aidha alisema pamoja na mambo mengine lakiji jumuiya ya ZSPCA inatambua mchango mkubwa wa wanyama kwa maisha ya mwanaadamu ikiwa ni pamoja na kuwapa misaada ya kuchukulia mizigo na chakula kwa maisha ya mwanaadamu.

Mambo mengine ni kutambua na kushukuru jinsi wanyama wanavyoyaboresha maisha yetu kwa ujumla, kusherehekea maisha ya wanyama.

Jumuiya ya ZSPCA imeanzishwa mwaka 2007 ambapo kwa Zanzibar ilianza kuadhimisha mwaka 2009 na ujumbe wa mwaka huu ni ‘Zanzibar bila ya ukatili kwa wanyama inawezekana, tuungane kulifanikisha’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.