Habari za Punde

BENI ZA MIEMBENI UNITED ZAFUNIKA KWALA

Na Mwajuma Juma

IKICHOMBEZWA na ngoma maarufu ya beni, timu ya Miembeni United jana ilimudu kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Miembeni SC, katika mchezo wa ligi kuu ya Sea gull uliochezwa kwenye uwanja wa Mao Dzedong.

Katika pambano hilo lililohudhuriwa na mashabiki wengi, washindi waliweza kujipatia mabao yao yote katika dakika 45 za kwanza, huku wapinzani wao wakibadilika na kupunguza idadi ya magoli mnamo kipindi cha pili.


Miembeni United ilianza kwa mashambulizi ya kasi yaliyowachanganya walinzi wa Miembeni Sports, ambapo mlinzi Ali Issa alijikuta akiizawadia timu hiyo bao kwa kujifunga katika harakati za kuokoa mnamo dakika ya tisa.

Mabao mengine ya washindi hao, yalifungwa na Suleiman Ali na Issa Hamad waolizifumania nyavu katika dakika za 17 na 30 mtawalia, kabla Amour Suleiman hajafunga kitabu kwa bao la mpira wa juu uliomshinda mlinda mlango wa Miembeni Sports na kuuacha ukitikisha nyavu.

Mabao hayo yalibaki hadi wakati wa mapumziko, ambapo wakongwe Miembeni asili walikianza kipindi cha pili kwa dhamira ya kubadilisha matokeo, na kufanikiwa kuandika bao la kwanza mnamo dakika ya 54 kupitia kwa Peter Frank.

Mchezaji huyo aliyeonekana kujituma na kuonesha mchezo safi, alidhihirisha ubora wake kwa kunongeza bao la pili kwenye dakika ya 72 ya mchezo, wakati ambao wachezaji wa Miembeni United walionekana kama waliotosheka na kuwaachia wapinzani wao kutawala mchezo katika dakika
za mwisho ingawa hawakuweza kuandika magoli zaidi.

Baada ya mchezo huo, jopo la waandishi wa habari walimchagua mchezaji Peter Frank kuwa bora kwa mchezo huo, na kuzawadiwa kikombe.

Kufuatia matokeo hayo, kocha msaidizi wa Miembeni SC Rashid Omar, alisema vijana wake walicheza vizuri, ingawa katika kipindi cha kwanza uzembe wa walinzi uliiponza timu yake, huku Said Omar Kwimbi akisema huo ni mwanzo mzuri na dalili ya kufanya vyema hadi mwisho wa msimu.

Katika mfululizo wa ligi hiyo, leo kutakuwa na mchezo kati ya timu ya Chuoni na Kikwajuni katika uwanja huo wa Mao Dzedong.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.