Habari za Punde

JAMII IONGEZE KASI VITA DHIDI YA UDHALILISHAJI

Na Juma Khamis

KESI 268 zinazohusiana na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto zimeripotiwa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu, lakini ni kesi 55 tu ndizo zilizokwenda mahakamani, ambapo nne kati ya hizo zimefutwa na mahakama kwa kukosekana ushahidi na moja mshitakiwa amepatikana na hatia.

Kesi hizo zinahusiana na ubakaji, kubaka kwa kundi, kutorosha, kulawiti, shambulio la kuumiza mwili, shambulio la hatari na shambulio la aibu.


Kesi 213 hazikufikishwa mahakamani kwa kile kilichodaiwa kukosekana ushahidi katika hatua za awali, watuhumiwa kutoroka na waathirika wa vitendo hivyo kutokuwa tayari kuendelea na kesi zao mahakamani.

Hata hivyo, takwimu ya kesi ambazo hazikufikishwa mahakamani ni kubwa, ikilinganishwa na zile zilizofikishwa mbele ya sheria.

Lakini sheria haizuii Idara ya Mwendesha Mashtaka (DPP) kutofikisha kesi ya jinai mahakamani kwa kigezo tu cha mtuhumiwa kutokuwepo mahakamani.

Akiwasilisha mada katika warsha ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na udhalilishaji kwa wanawake na watoto iliyowahusisha waandishi wa habari na wadau wengine, Fakihi Yussuf kutoka jeshi la polisi, alisema kesi hizo zimeripotiwa katika vituo sita vya mkoa huo.

Fakihi ambae ni Msaidizi wa Dawati la Wanawake na Watoto la Polisi Mkoa wa mjini Magharibi, alisema mwaka uliopita kesi 270 za aina hiyo ziliripotiwa.

Alisema kesi 69 zilikuwa za kutorosha, 33 za kubaka, 25 za kunajisi, shaka ya kuingilia 54, shaka ya mimba kesi 79 na kesi za kukashifu 10, ambapo 36 zilifikishwa mahakamani na hakuna hata kesi moja iliyopatikana na hatia, na kesi 233 hazikufikishwa mahakamani.

Hata hivyo, alisema tokea kuanzishwa kwa dawati la polisi, kumekuwa na mwamko kidogo kwa jamii na watu wamekuwa wakienda kuripoti kesi zao, lakini bado kuna changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa elimu ya ushauri na nasaha kwa watendaji wa dawati.

Alisema changamoto nyengine ni waathirika kutokuwa tayari kushirikiana na dawati katika utoaji wa ushahidi pindi kesi zinapofikishwa mahakamani.

Lakini wakichangia mjadala huo, washiriki wengi walilitupia lawama jeshi la polisi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kushughulikia kesi hizi na wakati mwengine kujifanya mahakakimu kwa kuzifanyia uamuzi pindi zinaporipotiwa.

Aidha baadhi ya vituo vimekuwa haviweki kumbukumbu ya kesi za aina hiyo zinaporipotiwa, na kituo kimoja kilichotajwa kuwa na tabia hiyo ni kile cha Mwanakwerekwe.

Washiriki pia waliwatupia lawama mahakimu wakidai kuwa hawataki kuumiza vichwa vyao, hali inayowafanya waathirika kutokuwa na imani na chombo hicho cha sheria.

“Mahakimu hawataki kujihangaisha, sijui tuseme nini kama kuna vishawishi vya rushwa au nini,” alisema Jamila Mahamoud kutoka chama cha wanasheria wanawake, ZAFELA.

Mwandishi Issa Yussuf kutoka Daily News, alisema kuna udhaifu wa uwajibikaji katika ngazi ya jamii, na kama jamii ingesimama kitu kimoja, basi vita hivi vingeshindwa.

Mzuri Issa kutoka TAMWA, yeye alisema nguvu kubwa iliyoelekezwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya, itumike sasa kukabiliana na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Katika mjadala huo, waathirika mbali mbali wa vitendo hivyo viouvu walipata fursa ya kutoa ushuhuda wao na kusababisha majonzi makubwa miongoni mwa waandishi wa habari.

Warsha hiyo imeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)kwa kushirikiana na Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.