• Wa kuiwakilisha Uzini kutambulika
• CUF nayo yakutana kujadili sakata la Hamad
Na Mwantanga Ame
KAMATI Maalumu ya NEC Zanzibar, inatarajiwa kukutana asubuhi ya leo ambapo pamoja na mambo mengine inafikiriwa, kikao hicho kitapokea matokeo ya kura za maoni za Uwakilishi wa Jimbo la Uzini pamoja na mapendekezo ya Kamati za Chama wilaya ya Kati na Mkoa.
Kikao hicho ambacho kinatarajiwa kuwa ni mwanzo wa kutambulikana hatma ya mgombea wa chama hicho atakayepewa jukumu la kusimama kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kufuatia kufariki kwa aliyekuwa
Mwakilishi wake Mussa Khamis Silima mwezi Agosti mwaka huu.
Kamati hiyo inayotarajiwa kukaa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Amani Abeid Karume, itapokea matokeo ya kura hiyo, baada ya majina ya wagombea 13 waliojitokeza kuwania nafasi kupitishwa katika vikao mbali mbali vya Chama.
Majina itayoyapokea pamoja na idadi ya kura walizopata akiwemo Mohammed Raza alieshika nafasi ya kwanza baada ya kupata kura (1,963), Othman Ali Maulid (643) , Khalifa Salum Suleiman (535), Abrazak Mussa Abdalla (32), Amour Abdalla Amour (15) na Fatma Ali Vuai (46).
Wengine ni Haji Ame Haji (280), Juma Kilala Masala (14), Khalifan Khamis Awadh (29), Matar Alu Salum (84), Paul Jembe Matiwili (46), Kanal Said Ali Hamad (36) na Suleiman Vuai Suleiman (29).
Wajumbe hao wanatarajiwa baada ya kupokea majina hayo wataweza kuyawekea alama maalum na kuyapeleka katika vikao vyengine vya Chama.
Majina hayo kabla ya kufikishwa katika kikao hicho tayari yamefikishwa katika kamati ya Siasa ya wilaya iliyokaa Disemba 14, kamati ya siasa ya Mkoa iliyokaa Disemba 17 ambapo hapo awali majina hayo yalifikishwa katika kamati ya Maadili.
Majina hayo yalifikishwa katika vikao hivyo baada ya Wanachama wa Jimbo la Uzini kupiga kura ya maoni kuchagua jina la Mwakilishi ataeweza kufikishwa katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar ili aweze kuwania
kiti hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo.
Uchaguzi huo unakuja baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mussa Khamis Silima, kufariki dunia pamoja na Mke wake walipokuwa wakielekea katika shughuli za Bunge Mjini Dodoma.
Kutokana na tukio hilo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar, imeitisha uchaguzi mdogo ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Febuari mwaka ujao.
Aidha, sekretarieti ya NEC itakutana Januari 4 na 5 na Kamati Kuu ya CCM kumthibitisha mgombea ataeteuliwa itakaa Januari 7 na 8.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, tayari imeeleza kuwa matayarisho ya uchaguzi huo yamekamilika kwa asilimia kubwa.
Wakati huo huo, kamati Tendaji ya Maadili ya CUF, imeanza kukutana jana huko Vuga Mjini Zanzibar kujadili kadhia ya wanachama 13, ambao wanashutumiwa kukiuka katiba ya chama hicho.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ambao wameelezwa kuanzisha uasi ndani ya Chama ni Mwakilishi wa Jimbo la wawi kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohammed.
Kamati hiyo pia itapokea na kujadili ripoti ya Tume ya Maadili ya chama hicho, ambayo itatolewa baada ya kufanyiwa usaili na uchunguzi wa tuhuma kwa wanachama hao 13.
No comments:
Post a Comment