Habari za Punde

MV SERENGETI YATOKA KIFUNGONI

Na Asya Hassan

BOTI ya Serengeti inayomilikiwa na Kampuni ya JAK Enterprises inatarajia kuanza safari leo usiku kutoka Unguja kuelekea Pemba baada ya kusimamishwa kwa karibu miezi mitatu kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati.

Meneja wa opereheni Ali Yussuf Abdallah alieleza hayo ofisini kwake Malindi alipokuwa akizungumza na gazeti hili alisema boti yao itafanya safari zake kama kawaida kutokana na kusawazishwa kwa matatizo yote ambayo yalipelekea kusimamishwa kwa safari zake.


Alisema kuzuiliwa kwa boti yao kunatokana na Mkurugenzi amri wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari, ambaye mara mbili alitoa agizo la kusitishwa kwa safari za boti hiyo.

Meneja Ali alisema kutokana na kuzuiliwa huko mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana nae kwa ajili ya kutaka kuona mapungufu yanawekwa bayana ili yaweze kufanyiwa kazi.

“Mkurugenzi tulikuwa na mawasiliano nae mara kwa mara kutokana na matatizo ya boti hiyo lakini alikuwa akiturejesha nyuma kwa biashara zetu”, alisema Meneja huyo.

Alisema kuwa boti hiyo inatarajia leo kuanza safari baada ya kukarabatiwa na kuchunguzwa na SUMATRA kutoka Tanzania bara na kuthibitisha kuwa haina kasoro yoyote.

Meneja Ali alifahamisha kuwa serikali inatakiwa kuwa makini kutokana na taarifa mbalimbali wanazopelekewa na watumishi wao kwani wamekuwa na taarifa za kubabaisha mara kwa mara.

Alisema upo umuhimu kwa serikali kutafuta ajira mbadala kwa wananchi wa Pemba ili kuwapunguzia tatizo la usafiri kwani boti yao imekuwa ikitowa huduma kubwa ya kubeba chakula.

Alieleza kuwa Serengeti ni boti ambayo inahimili purukushani za bahari na ndio inayochukuwa abiria wengi na mizigo.

Boti ya Serengeti ni boti ambayo inayochukuwa abiria 850 na mizigo karibia tani 200 inatarajiwa kufanya safari wiki mara 3 kutoka Unguja kwenda Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.