Habari za Punde

SERIKALI KUWAKATAA WAKURUGENZI 'MIZIGO'

Na Mwantanga Ame

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, amesema serikali haitakubali kuwa na Wakurugenzi Mipango na Sera wasiofahamu wajibu wao.

Waziri huyo alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya uwezeshaji kwa Wakurugenzi wanaoshughulikia Mipango, Sera na Utafiti katika taasisi za serikali yaliyofanyika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort na
kufadhiliwa na Jumuia ya Madola.


Waziri Mzee, alisema Wakurugenzi Mipango katika serikali ni kiungo muhimu cha kutekeleza malengo ya serikali na haiwezekani serikali ikabeba aibu na fedheha ya watendaji wasioelewa namna ya kuitekeleza.

Alisema inasikitisha katika karne hii kuna baadhi ya Wakurugenzi Mipango na Sera ndani ya serikali hawafahamu mpango wowote wa taasisi anayoisimamia na Wizara nyengine watendaji wake wanashindwa kuwajibika katika utendaji wao.

Alisema baadhi ya watumishi hao wanashindwa hata kufahamu wajibu wao na kuuliza taasisi nyengine zinawajibika vipi katika majukumu yake.

Akitoa mfano alisema Tanzania hivi sasa imo katika utekelezaji wa mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini uliowekewa mkakati wa kuongeza uchumi kwa asilimia nane lakini imeshindwa kulifikia lengo
hilo.

Alisema Zanzibar imo katika utekelezaji wa mkakati wa dira ya 2020 ambao uliwekwa mwaka 2000 wenye malengo kadhaa inayotegemewa utekelezaji wake kusimamiwa na Wakurugenzi Mipango wa Taasisi za
serikali

Alisema moja ya kasoro kubwa iliyojitokeza katika sekta ya kilimo ambayo ina idadi kubwa ya wazanzibari waliojiari katika kazi hizo, lakini wataalamu walishindwa kufahamu mahitaji ya kuinua kilimo vipi
yawekewe utaratibu mzuri ili yaweze kuwa na tija kwa jamii na taifa.

Alisema takwimu za Kaya zimeonesha bado tatizo la umasikini lipo Zanzibar, kwani katika kipindi cha mwaka 2004 hadi 2005 umasikini ulifikia asilimia 49 na mwaka 2010 ulifikia asilimia 44.10.

Kutokana na hali hiyo, Wziri huyo, alisema ipo haja kwa Wakurungenzi Mipango waliopewa jukumu hilo kuhakikisha wanabadilika kiutendaji kwa kuhakikisha wanaandaa mipango isiyoweza kuitia hasara serikali wala jamii.

Waziri huyo alisema serikali hivi sasa imeshafanya mabadiliko ya kuwa na Tume ya Mipango ambayo itawawezesha Wakurugenzi wote wa SMZ kukaa pamoja na kuona vipi wanatekeleza majukumu yao na kujua nini serikali yao inachokitaka.

Aidha, Waziri huyo alikemea tatizo la watendaji kutotaka kubadilika kwa kuendeleza utaratibu wa kufanya kazi kwa mazoea huku kukiwa hakuna tija wanayochangia katika kuendesha shughuli za serikali.

Alisema hilo ni moja ya jambo la kuzingatiwa kwa vile Zanzibar hivi sasa inahitaji kufanya shughuli zake kwa kuyaelewa malengo yaliomo katika nchi za SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mashirika mengine
ya kimataifa.

Kuhusu athari za kutegemea bajeti za nje, Waziri huyo, pia aliomba suala hilo waliangalie kwa kina kwani baadhi ya watu huja na mipango ambayo hushindwa kuitekeleza miradi inayoombewa fedha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.